Serikali haitavumilia udanganyifu, kuchezea mifumo maalum ya afya

By Christina Mwakangale , Nipashe
Published at 11:21 AM Sep 12 2024
Waziri wa Afya, Jenista Mahagama.
Picha:Mtandao
Waziri wa Afya, Jenista Mahagama.

SERIKALI imesema haitavumilia udanganyifu na uchezeaji wa mifumo ya huduma za matibabu kupitia bima ya afya itakayosimamiwa na mfuko maalum, kuelekea huduma ya Afya kwa Wote.

Waziri wa Afya, Jenista Mahagama, aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam baada ya kufanya ziara katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) na kwamba lengo ni kuboresha Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) na ufanye majukumu yake ipasavyo.

“Kwa kweli tutakuwa wakali na mimi nitakuwa mkali kabisa, kusimamia na kuhakikisha fedha zitazotumika kusimamia matibabu kutoka katika mfuko zinatumika kwa wakati, mahala sahihi. NHIF tumeona hapo katikati ulivyoyumba, kipindi hiki cha mpito tunaiboresha kwanza.

“Hatuko tayari kumvumilia mtu ambaye atachezea mifumo yetu. Huko nyuma kumekuwa na udanganyifu na hatutakuwa tayari. Afya ni usalama na ikiwa bora na yenye ustawi ni usalama. Lazima tuwe na mfumo wa ku-track (kufuatilia) tangu mgonjwa anapokelewa, anaanza huduma hadi anamaliza,” alisema. 

“Mfumo wa Afya kwa Wote unalenga kuwafikia wananchi wote, tunaweza kuwa na tiba nzuri sana na isipowafikia wanyonge inakuwa haina maana. Tunalenga pia kuzitambua hospitali zinazofanya vyema kwenye utoaji huduma, lakini baada ya kuwezeshwa katika ubobezi,” aliongeza.  

Pia alisema JKCI ni mfano wa kuigwa kutokana na kutoka matibabu bobezi na ya kibingwa kwa Kanda ya Afrika Mashariki, Kati na Kusini huku ikipokea wageni wakiwamo watalii. 

“Nilichoona ni bado huduma za matibabu ni kubwa na lengo ni huduma kumfikia kila mmoja. Mfumo wa Bima ya Afya kwa Wote ni maono ya Rais nami nitafanyia kazi hilo, bima hii iwezeshe kila mmoja kufikiwa. Tunamalizia kanuni ili wananchi waanze kutumia Afya kwa Wote,” alisema Mhagama.  

Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Dk. Peter Kisenge, alisema uwekezaji uliofanywa na serikali umeongeza upatikanaji wa huduma bora na za kibingwa na kwamba kupitia mpango wa Tiba Mkoba ya Rais Samia, imewezesha kuwafikia wananchi zaidi ya 17,000 nchi nzima.

“Mpango huo uliowezeshwa na Rais umesaidia kuwapatia wagonjwa wenye matatizo na hapa JKCI tunafanya operesheni nne hadi tano kwa siku. Kwa wagonjwa wa nje (OPD), tunayaona takribani wagonjwa 500 kwa siku,” alisema Dk. Kisenge. 

Aliongeza kuwa tayari taasisi hiyo imepokea wagonjwa kutoka nchi takribani 20 na pia malengo ni kuimarisha teknolojia, ili kuwafikia wagonjwa wengi zaidi na tayari JKCI katika robo mwaka wagonjwa wapatao 300 wametokana na tiba utalii.