RC Mara akemea wanaojihusisha na uvuvi haramu Ziwa Victoria

By Sabato Kasika , Nipashe
Published at 04:34 PM Feb 18 2025
Kanali Evans Mtambi akisalimiana na baadhi ya wakazi wa Kijiji cha Kwikuba.
Picha:Mpigapicha Wetu
Kanali Evans Mtambi akisalimiana na baadhi ya wakazi wa Kijiji cha Kwikuba.

Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Michael Mtambi, ametoa onyo kali kwa watu wanaojihusisha na uvuvi haramu katika Ziwa Victoria, akiwataka kuacha mara moja kabla ya kuchukuliwa hatua za kisheria.

Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika jana katika Kijiji cha Kwikuba, Wilaya ya Musoma, Kanali Mtambi alisisitiza kuwa uvuvi haramu haukubaliki na unahatarisha mustakabali wa rasilimali za uvuvi katika mkoa huo.

"Wananchi wa Mkoa wa Mara muungane na kukemea uvuvi haramu kwa kutoa taarifa zitakazosaidia kuwakamata wahusika ili wachukuliwe hatua za kisheria," alisema Kanali Mtambi.

Alibainisha kuwa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Mara inajiandaa kufanya operesheni maalum ya kudhibiti uvuvi haramu, ambapo wote wanaojihusisha na vitendo hivyo watakamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.

Kanali Mtambi alionya kuwa uvuvi haramu umeleta athari kubwa kwa mazingira ya Ziwa Victoria, ikiwemo kupungua kwa idadi ya samaki, hali ambayo imechangia kufungwa kwa viwanda vya kuchakata minofu ya samaki vilivyokuwepo katika mkoa huo.

Eneo la wazi ambalo ulifanyika mkutano wa mkuu huyo wa mkoa.
"Tukidhibiti uvuvi haramu, idadi ya samaki itaongezeka, na hivyo kuvutia wawekezaji wa viwanda vya kuchakata samaki. Hili litasaidia kuinua uchumi wa mkoa wetu," aliongeza.

Aidha, alisema kuwa serikali inaendelea na ukarabati wa Uwanja wa Ndege wa Musoma ili kurahisisha usafirishaji wa samaki na bidhaa nyingine kwenda maeneo mbalimbali ndani na nje ya nchi.

"Uwekezaji huu wa serikali hauna maana kama ndege zitakuja Musoma kusafirisha abiria pekee, bila mizigo kama samaki. Ni lazima tuhakikishe tunalinda rasilimali zetu," alisema.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Juma Chikoka, alisema wilaya hiyo imeanzisha operesheni maalum ya kupambana na uvuvi haramu na wamejipanga kuhakikisha tatizo hilo linatokomezwa.

"Operesheni hii itawagusa wote wanaojihusisha na uvuvi haramu. Tunawakaribisha wananchi wote wenye taarifa kuhusu watu wanaofanya vitendo hivyo ili tuweze kuzifanyia kazi," alisema Chikoka.

Aliongeza kuwa wilaya hiyo inatoa kipaumbele kwa sekta za uwekezaji, ikiwemo kilimo, uvuvi, ufugaji na uchimbaji wa madini, ambazo ni nguzo muhimu za uchumi wa wananchi wake.

"Pia, katika mikopo ya vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, miradi ya uzalishaji mali imepewa kipaumbele ili kusaidia kukuza uchumi wa wananchi," alisisitiza Chikoka.