Mtaalamu ataja chanzo ongezeko matukio ya nyuki kushambulia watu

By Thobias Mwanakatwe , Nipashe
Published at 11:14 AM Sep 11 2024
Nyuki.
Picha:Mtandao
Nyuki.

MKURUGENZI Mtendaji wa Kijiji cha Nyuki Co.Limited amewataka wananchi kuwekeza katika sekta ya ufugaji nyuki ili kukabiliana na ongezeko la nyuki ambao wameanza kuingia katika makazi ya watu, nyumba za ibada na kuwashambulia watu, wakiwajeruhi na wakati mwingine kusababisha vifo.

Philemon Kiemi alisema hayo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari kufuatia tulio la hivi karibuni la watu kushambuliwa na nyuki eneo la Mbweni, Dar es Salaam na kuwajeruhi. 

Alisema hivi sasa kuna ongezeko kubwa la makundi ya nyuki ambao wanazagaa kwenye makazi ya watu, misikiti, makakisa, shule, minara ya simu na maeneo mengine na hali hii inatokana na kwamba wamekosa sehemu ya kwenda kwa sababu hakuna mazingira maalum yaliyoandaliwa kuwatunza. 

"Matukio ya watu kushambuliwa na nyuki hivi karibuni yameripotiwa kutokea katika mikoa ya Dodoma, Dar es Salaam, Singida, Kagera na Shinyanga, hali hii inajitokeza kwa sababu makundi ya nyuki ambayo yalitakiwa kufugwa na binadamu, lakini binadamu hawa hawafanyi jitihada za kuwatengenezea nyuki makazi, ikiwamo mizinga," alisema. 

Kiemi alisema njia pekee ya kuwafanya nyuki kurudi msituni ni kutengeneza mizinga ya kisasa itakayowavutia kuingia humo na kutenga maeneo maalum ya kuwafuga ambapo jitihada hizo zisipochukuliwa, matukio ya watu kushambuliwa na makundi ya nyuki yataendelea. 

Alisema katika Mkoa wa Singida pekee, kunakadiriwa kuwa na makundi ya nyuki 900,000 lakini makundi ambayo yamo katika mizinga ni 240,000, hivyo makundi yaliyobaki, zaidi 600,000 yanaishi katika majabali, miti, makazi ya watu, shuleni, misikitini na kanisani. 

Kiemi alisema katika kipindi cha takribani miaka 10, zaidi ya watu 10 wamefariki dunia mkoani Singida kutokana na kushambuliwa na nyuki. 

"Safari wanazofanya nyuki kwenda kutafuta maji na safari  zinafanana na safari wanazotumia kwenda kutafuta malisho, hivyo sisi watalaamu tumeamua kutengeneza mizinga ambayo ina sehemu ya kuweka maji ili kuwapunguzia safari nyuki kwenda kutafuta maji," alisema. 

Mtaalamu huyo alisema hatua hiyo itamwezesha mkulima kuvuna asali zaidi ya mara moja. 

Kiemi alisema njia nyingine ya kukabiliana na matukio ya kushambuliwa na nyuki ni wananchi kupewa elimu, mtu anaposhambuliwa na nyuki anatakiwa kusaidiwa vipi ili asipate madhara makubwa zaidi.

 "Mtu akishambuliwa na nyuki, hatua ya kwanza ni kumwondolea miba ya nyuki ili sumu isiingie zaidi mwilini mwake na hatua ya pili ni kumpa maji na kumpeleka kwenye chumba chenye giza.

 "Watu wasichukulie nyuki kuishi kwenye dari ni baraka, hapana! Ni sababu wamekosa sehemu maalum pa kwenda," alisema.

 Kiemi alisema kuwa kutokana na ongezeko hilo la nyuki, wananchi hivi sasa wajenge tabia ya kutembea na vifaa vya kujikinga na nyuki wanapokwenda kazini na kwenye magari, kama tahadhari ya kukabiliana nao wanaposhambuliwa.

 Alisema Kijiji cha Nyuki Co. Limited kimejipanga kuwafundisha asilimia 75 ya Watanzania ili waweze kuingia katika sekta ya ufugaji nyuki na pia waweze kulima mazao kama alizeti ambayo hayaathiri nyuki.

 Alisema kuwa hivi sasa wananchi wengi wameanza kujitokeza kuingia katika sekta ya kufuga nyuki baada ya kutambua kuwa ufugaji wa nyuki hauna gharama sana, ni kuwa na mzinga tu.