Timu 5 bado hazijaonja ladha ya ushindi Ligi Kuu

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 09:16 AM Sep 24 2024
 Ligi Kuu Tanzania Bara
Picha: Mtandao
Ligi Kuu Tanzania Bara

WAKATI Ligi Kuu Tanzania Bara ikiingia raundi ya tano, jumla ya timu tano bado hazijaonja ladha yoyote ya ushindi.

Timu hizi ni Prisons, Pamba Jiji, JKT Tanzania, Coastal Union na KenGold, zimecheza michezo tofauti, zikiwa hazijashinda mechi yoyote ya Ligi Kuu msimu huu.

Kwa mujibu wa dawati letu la takwimu, Prisons ambayo iko nafasi ya tisa kwenye msimamo wa ligi, imecheza michezo minne bila kushinda, ikitoka sare mechi zote na ina pointi nne.

Pamba Jiji, imeshatimiza michezo mitano mpaka sasa ikiwa imepanda daraja msimu huu, lakini haijaonja ladha ya ushindi wa Ligi Kuu, ikitoka sare nne na kupoteza mmoja, ikiwa na pointi nne kwenye nafasi ya 10 ya msimamo.

JKT Tanzania imecheza michezo mitatu ambayo yote imetoa sare, ikiwa na pointi tatu na inashika nafasi ya 13.

Coastal Union mpaka sasa imeshacheza michezo minne, ikitoka sare moja tu na kupoteza mitatu, ikikamata nafasi ya 15 na KenGold inayoshika mkia, ikiwa imecheza mechi nne, ikipoteza zote na haijavuna pointi mpaka sasa.

Singida Black Stars ndiyo timu iliyoshinda michezo yote iliyocheza kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara mpaka sasa.

Timu hiyo imeshinda michezo minne iliyocheza kwenye ligi na kuwa na ushindi wa asilimia 100.

Ilianza ligi kwa kuifunga KenGold mabao 3-1, ikaichapa Kagera Sugar bao 1-0, ikapata ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya KMC, kabla ya kuifunga Pamba Jiji bao 1-0.