Msalala yatenga milioni 78 kwa ajili ya lishe

By Shaban Njia , Nipashe
Published at 04:34 PM Nov 02 2024
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Msalala Rose Manumba akizungumza na wananchi wa kata ya segese wakati wa maadhimisho ya siku ya lishe duniani pembeni yake ni watumishi wa halmashauri hiyo.
PICHA; SHABAN NJIA.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Msalala Rose Manumba akizungumza na wananchi wa kata ya segese wakati wa maadhimisho ya siku ya lishe duniani pembeni yake ni watumishi wa halmashauri hiyo.

HALMASHAURI ya Msalala wilayani kahama mkoani Shinyanga, imetenga Sh. milioni 78 fedha kutoka mapato ya ndani ya halmashauri hiyo kwa ajili ya kuchangia shughuli mbalimbali na kupambana na tatizo la udumavu na utapiamlo kwa watoto wadogo chini ya miaka mitano na wajawazito.

Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Rose Manumba aliyabainisha haya wakati akizungumza na wananchi wa Kata ya Segese katika maadhimisho ya siku ya lishe Duniani na kuwasisitiza kuandaa vyakula vyenye lishe kwa kuzingatia makundi ya vyakula yanayopatikana kwa urahisi kwenye maeneo yao. 

Alisema,kwa kuzingatia umuhimu wa lishe kwa watoto na wajawazito wametenga kiasi cha Sh.milioni 78 kwa ajili ya kupambana na utapiamlo na udumavu na watafikiwa na kuelimishwa namna ya kuandaa vyakula vyenye lishe kwa kuzingatia makundi ya vyakula vinavyopatikana kwa urahisi. 

“Mtoto anatakiwa kupata vyakula vyenye lishe na sio kula ovyo, tunalima sana mazao ya chakula na biashara lakini hatufahamu namna ya kuvindaa na kusababisha kuwa na watoto wenye udumavu na utapiamlo…..Kumbukeni hata mjamzito anatakiwa kula vyakula vyenye lishe ili ajifungue mtoto mwenye afya” aliongeza. 

Manumba alisema, kushiba pekee sio lishe bora bali wanatakiwa kuzingatia namna sahihi ya uandaaji wa chakula kwa kuzingatia makundi yote ya vyakula na kuwataka maafisa lishe kuhakikisha wanawatembelea wananchi kila kata na kuwaelimisha namna ya kuandaa kulingana na aina ya vyakula wanavyozalisha kwenye maeneo yao. 

Nae Ofisa Lishe wa Halmashaueri hiyo Peter Ngazo alisema, watahakikisha wanayafikia pia makundi ya akinababa, vijana na kuyafahamisha makundi ya vyakula vyenye lishe na namna ya kuandaa ili nao wapate wasaa wa kuwahimisha wake zao na watatumia aija ya vyakula vinavyopatakana kwenye maeneo yao kwa urahisi. 

Hata hivyo alisema, vyakula vinavyotakiwa ni vile vya makundi ya mafuta, matunda, Asili ya wanyama, jamii ya mikundi, mbogamboga, nafaka, mizizi pamoja na ndizi mbichi na vyote vinapatikana kwenye maeneo yao isipokuwa ni kutokuwa na elimu ya namna ya kuviandaa tu. 

Alisema, mtoto asipopata lishe bora akiwa mdogo ipasavyo anatakuwa hana uwezo wa kutunza kumbukumbu kwa kile anachofanywa au kuelekezwa hata katika safari yake ya masomo atashindwa kufanya vema kwenye mitihani yake ya mwisho hivyo kila mzazi atakiwa kuzingatia suala la lishe na kulipatia kipaumbele.

3 (8).JPG 212.69 KB