Mpango mkakati wa kusaidia wakulima wa shayiri wazinduliwa

By Augusta Njoji , Nipashe
Published at 09:40 AM Apr 26 2024
Mkurugenzi Msaidizi kutoka Idara ya Maendeleo ya Mazao, Wizara ya Kilimo, Beatrice Banzi.
Picha: Augusta Njoji
Mkurugenzi Msaidizi kutoka Idara ya Maendeleo ya Mazao, Wizara ya Kilimo, Beatrice Banzi.

MPANGO mkakati wa kusaidia wakulima wa zao la shayiri Tanzania umezinduliwa ili kuongeza uzalishaji wa zao hilo na kukidhi soko la viwanda vya ndani na biashara katika ukanda la ndani.

Akizungumza mara baada ya kuzinduliwa kwa mkakati huo, Mkurugenzi Msaidizi kutoka Idara ya Maendeleo ya Mazao, Wizara ya Kilimo, Beatrice Banzi amesema mkakati huo  unaweka kipaumbele maeneo matano.

Amesema maeneo hayo ni upatikanaji wa mbegu, kuwahamsisha na kuwaunganisha wakulima kupitia ushirika na mifumo mingine na kuboresha masuala ya miundombinu ikiwamo masoko ya zao la shairi.

“Eneo lingine la mpango huu ni kuboresha sera na sheria katika masuala ya uzalishaji na biashara ya zao la shayiri na masuala ya kilimo cha mkataba, kwa sasa kumekuwa ni kama mwiba kwa wakulima, mnunuzi na mzalishaji hivyo kupitia mkakati huu tunakwenda kutibu hili tatizo la kwa nini mikataba yetu inakuwa haina tija kati ya mkulima, mnunuzi na mzalishaji. Hivyo utekelezaji wa mpango mkakati huu utafuatwa hatua kwa hatua utaongeza uzalishaji wa zao la shayiri,”amesema

Naye, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Nafaka na Mazao Mchanganyiko(COPRA), Irene Mlola amesema mkakati huo umelenga kuhakikisha kampuni ya bia ya TBL inanunua zao hilo kwa wakulima na shayiri inayozalishwa ikidhi mahitaji. 

Naye, Mwakilishi wa Shirika la IFC, Sam Nganga amesema taasisi yake itaendelea kusaidia mpango huo ili kuwasaidia wakulima kuondokana na tatizo la upatikanaji wa fedha, uzalishaji mdogo wa mazao na kuzalisha kwa ubora.