Waziri wa Madini, Anthony Mavunde amekutana na Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Peak Resources Ngualla Company ya nchini Australia ( PRNG) Bardin Davis, yenye umiliki wa hisa asilimia 84 kwenye mradi wa Uchimbaji Madini Mkakati ya Rare Earth Elements.
Katika kikao hicho kilichofanyika leo Aprili 18, 2024 jijini Dodoma, Bardin ameambatana na Afisa Mkuu wa masuala ya Fedha ya kampuni hiyo, Phil Rundell, pamoja na Mkurugenzi wa Mamba Minerals Corporation Limited ( MML) yenye ubia na Serikali, Ismail Diwani.
Katika kikao hicho, Mtendaji Mkuu wa PRNG Bardin amemweleza Waziri Mavunde kuhusu maendeleo ya mradi huo na kueleza kuwa hivi sasa upo katika hatua ya kufanya tathmini ya fidia ya wananchi wanazunguka mgodi ikiwemo uendelezaji wa utafiti wa madini ya mkakati aina ya niobium, fluorspar na phosphate.
Aidha, Bardin ametumia kikao hicho kuishukuru wizara kupitia Tume ya Madini kwa kuridhia kuongeza ukubwa wa leseni ya kampuni hiyo.
Akizungumza katika kikao hicho, Waziri Mavunde ameusisitiza uongozi wa kampuni hiyo kufuata masharti ya leseni waliyopewa ikiwa ni pamoja na kuzingatia matakwa ya Sheria ya Madini na kusisitiza kuhusu umuhimu wa madini hayo kusafishwa hapa hapa nchini.
Madini ya rare earth elements yanayotumika kutengeza sumaku kwenye mota za magari ya umeme , betri za magari ya mseto na umeme;na vitu vingine mbalimbali vya umeme.
Kampuni ya Mamba Minerals inayomiliki leseni kubwa ya uchimbaji yenye jina la Rare Earth Elements ilitolewa tarehe 25 Aprili, 2023.
Mradi wa uchimbaji madini hayo upo kijiji cha Ngualla, Mkoani Songwe.
Katika mradi huo, Serikali ya Tanzania ina miliki asilimia 16 za hisa zisizohamishika.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED