KITUO cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi (PPPC), kimesema mwisho wa mwezi huu kitatuma wataalamu kwenda Manispaa ya Ilemela jijini Mwanza, kwa ajili ya kuangalia maeneo muhimu ya miradi ya ubia.
Uamuzi huo umekuja baada ya madiwani wa Manispaa ya Ilemela kutembelea PPPC jana kujifunza namna kinavyofanyakazi na watakavyotumia rasilimali ardhi waliyonayo kutekeleza miradi ya ubia baina ya sekta binafsi na sekta ya umma.
Mkurugenzi Mkuu wa PPPC, David Kafulila aliyasema hayo jana wakati akizungumza na madiwani wa manispaa hiyo ambao pia miongoni mwao alikuwapo Mbunge wa Jimbo la Ilemela, Angelina Mabula, Meya wa Ilemela, Renatus Mulunga na Mwenyekiti wa CCM, Yusuph Bujiku.
Alisema uamuzi wa manispaa hiyo ni mzuri kwa kuwa wataendesha miradi kwa kutumia mtaji wa umma ambao unapatika kwa ubia na sekta binafsi.
"Mmefanya uamuzi sahihi kuja kututembelea, mjifunze kwa kuona mradi wetu wa DDC ambao unatekelezwa kwa PPP ila tuna miradi mingine iliyopo katika hatua mbalimbali 82, na maeneo mengi ambayo mnaweza kuyaendeleza kwa mtaji wa umma," alisema.
Kafulila alisema ubia ni ndoa ya ushirikiano na si ubinafsishaji kama inavyoelezwa na kwamba miradi ya ubia yote ni mali ya serikali kabla, wakati na baada na sekta binafsi inaingiza mtaji na kuendeleza.
Aidha, alizitaja sababu za ubia kuwa ni kuvuna mtaji wa sekta binafsi kwa ajili ya kutekeleza miradi ya serikali badala ya kukopa na kwamba fedha ambayo serikali ingetumia kuwekeza itatekeleza miradi mingine maeneo ambayo sekta binafsi haijaona fursa.
Alizitaja sababu nyingine za uwekezaji kuwa ni kuvuta mitaji kutoka sekta binafsi, kuvuta teknolojia ambayo utafiti unaonesha ni sekta binafsi imepiga hatua eneo hilo.
Nyingine ni kuongeza ufanisi wa kiutendaji kwa kuwa sekta binafsi inamudu kusimamia mambo yake kwa ufanisi mkubwa bila urasimu kuliko ambayo serikali ingefanya.
Nyingine ni uamuzi wa kiufanisi, huku akitoa mfano kuwa zipo sekta binafsi huajiri wakurugenzi wa mshahara mkubwa kwa kuwa wanachokitafuta ni ufanisi, kwa PPP sekta binafsi inaweza kununua mtaalamu mwenye ufanisi mkubwa kwenye utekelezaji wa miradi.
Kwa mujibu wa Kafulila, mahitaji ya binadamu yanaongezeka kila siku kuliko uwezo wa serikali yoyote duniani kuyamudu, na kwamba chanzo cha mapato cha serikali ni kodi na mikopo, haiwezi kumudu kuyatimiza bila PPP.
"Uzoefu unaonyesha kuwa serikali haiwezi kufikia matarajio kwasababu inategemea kodi na mikopo. Deni la dunia kwa sasa ni dola trilioni 300 huku uchumi ukiwa ni Dola trilioni 110 ambayo ni mara tatu ya uchumi," alisema.
"Huwezi kutimiza mahitaji kwa kukopa, lazima ualike sekta binafsi ije na mitaji yake itekeleze, kwa kutumia PPP unatekeleza miradi bila kugusa bajeti na kupunguza shinikizo kwenye vitabu vya serikali. Ilemela mmefanya uamuzi sahihi," alisema Kafulila.
Aidha, alisema michuano ya AFCON 2027 ni fursa kwa Tanzania kutumia PPP kujenga viwanja na huduma nyingine muhimu na kwamba ni muhimu ikaangaliwa kama fursa ya kiuchumi.
Naye Meya wa Manispaa ya Ilemela, Renatus Mulunga, alisema wapo tayari kwa kuwa wana maeneo mengi ambayo yanaweza kutumika kutekeleza miradi kwa ubia na ndio sababu ya kujifunza ili wafanye uamuzi sahihi anapopatikana mwekezaji.
Mbunge wa Jimbo la Ilemela, Angelina Mabula, alisema Manispaa hiyo ilishatenga maeneo ila haijapata mwekezaji na kwamba wameona PPP ndio njia sahihi.
"Tuna eneo la Mahombolo tunaweza kujenga viwanja hasa kwa ajili ya AFCON, tunahitaji kituo cha mabasi na soko la kisasa, hii hatuwezi kutekeleza kwa bajeti za manispaa bali kwa PPP," alisema.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED