Gari lenye shehena la mirungi lakamatwa

By Marco Maduhu , Nipashe
Published at 10:54 AM May 29 2024
Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Janeth Magomi.
Picha: Mtandaoni
Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Janeth Magomi.

JESHI la Polisi mkoani Shinyanga limekamata gari iliyobeba dawa za kulevya aina ya mirungi viroba 25, huku dereva akitokomea kusikojulikana.

Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Janeth Magomi alibainisha hayo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari na kueleza kuwa jeshi hilo linaendelea kumsaka dereva wa gari hilo pamoja na mmiliki.

Alisema mirungi hiyo ilikamatwa katika gari moja ambalo liligonga ng’ombe maeneo ya Bugweto Manispaa ya Shinyanga, na askari walipofika eneo la tukio na kufanya ukaguzi ndipo wakakuta viroba 25 vya mirungi, huku dereva akikimbia.

Aidha, alisema kuwa kupitia msako uliofanyika kuanzia Aprili 17 hadi Mei 27 mwaka huu walikamata dawa za binadamu zilizoisha muda wake zilizokuwa zikiuzwa katika mojawapo ya duka la dawa katika Manispaa ya Shinyanga.

“Tulikamata pakiti 86 za dawa hizo ambapo mtuhumiwa anaendelea kushikiliwa kwa hatua zaidi za kisheria,”alisema Magomi.

 Alitaja bidhaa nyingine zilizokamatwa kuwa ni pamoja na televisheni moja, mzani mmoja, redio moja, pikipiki 16 pamoja na pombe haramu aina ya gongo lita 20.

Kuhusu usalama barabarani, Kamanda Magomi alisema walikamata makosa 6,320 upande wa pikipiki, huku magari yakiwa ni 4,847, bajaji na pikipiki 1,473 ambapo wahusika waliwajibishwa na kulipa faini ya papo kwa papo.