JESHI la Polisi nchini limesema limeanza uchunguzi dhidi ya tukio la Mjumbe wa Sekretarieti ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Ally Kibao, anayedaiwa kutekwa wakati akisafiri kwa basi la Tashrif.
Jana, Katibu Mkuu wa CHADEMA, John Mnyika, alitoa madai hayo mbele ya vyombo vya habari, huku Msemaji wa Jeshi la Polisi, Naibu Kamishna wa Polisi (DCP), David Misime, akieleza kuanza kwa uchunguzi huo.
Katika taarifa yake, Misime alisema kuna taarifa zimesambaa katika mitandao ya kijamii zikieleza kuwa juzi jioni maeneo ya Tegeta, Dar es Salaam, Kibao akiwa safarini na basi la Tashrif, alishushwa na kuchukuliwa na watu wasiojulikana majina yao.
“Leo (jana) tumesikia taarifa kuhusiana na tukio hilo kupitia vyombo vya habari iliyotolewa na Mnyika. Jeshi la Polisi lingependa kutoa taarifa kuwa lilipokea taarifa hiyo na kuanza uchunguzi wa kubaini kilichotokea, chanzo chake na watu waliohusika ni akina nani,” alisema Misime katika taarifa hiyo.
Awali, akizungumzia tukio hilo, Mnyika alilitaka jeshi hilo kueleza aliko Kibao.
Mnyika alisema alipokea taarifa za tukio hilo juzi saa 12 jioni za madai ya kutekwa kwa Kibao katika eneo la Kibo Complex Tegeta, alipokuwa akisafiri kuelekea Tanga anakoishi.
“Akiwa amepanda basi la Tashrif lenye namba za usajili T 343 EES, lilipofika maeneo hayo likazuiwa na magari mawili nyeupe aina ya Toyota Landcruiser na gari dogo lingine yakiwa hayana nembo yoyote.
“Wakashuka watu kutoka humo wakiwa na silaha moja kati yao akaenda katika kioo cha mbele kwa dereva, wawili wakaingia ndani, wengine wakabaki nje walikwenda moja kwa moja katika siti yake wakamchukua kwa nguvu.
“Wakati wanashuka akaongezeka mwingine mmoja aliyekuwa ndani ya gari whilo akaungana na wenziwe na kwa taarifa nilizonazo wakati wanamshusha walimpiga,” alidai Mnyika.
Katibu Mkuu huyo alisema mpaka sasa hawajui mwenzao yuko wapi na ana hali gani.
“Tumetuma mawakili wa chama Kituo Kikuu cha Polisi ili tujue yuko wapi, lakini mpaka sasa hatujapata taarifa yoyote ya wapi yupo. Nitoe wito kwa Mkuu wa Jeshi la Polisi aeleze iwapo alitekwa, sababu za kumteka, yuko wapi na ana hali gani,” alisema.
Mnyika alisema msimamo wa chama kutokana na uzito wa kushamiri kwa vitendo hivyo mathalani uchaguzi unapokaribia, wameanza maandalizi ya kikao cha chama ili kutafakari hali ya usalama nchini na kufanya uamuzi wa pamoja na kisha wataeleza hatua watakazochukua.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED