Viongozi Wakuu wa Chama cha ACT Wazalendo wanatarajia kufanya awamu ya pili ya ziara ya maandalizi ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa katika mikoa 21 ya Tanzania Bara inayotarajiwa kuanza Septemba,11 2024.
Naibu Katibu Idara ya Habari, Uenezi na Mahusiano na Umma wa chama hichi, Shangwe Ayo akizungumza na wanahabari leo Septemba 08,2024 amesema awamu ya kwanza ya ziara hiyo ya #Miezi10 #WanachamaMilioni10 ilifanyika kuanzia Julai 22, 2024 hadi Agosti 17,2024 ikihusisha majimbo 125 yaliyopo katika mikoa 22.
Amesema kama ilivyokuwa kwenye awamu ya kwanza ya ziara hiyo, awamu hii ya pili itawahusisha Kiongozi wa Chama Dorothy Semu,ambaye atatembelea maǰimbo 25 kwenye Mikoa ya Pwani, Dodoma, Manyara, Singida, Manyara, Arusha, Kilimanjaro na Tanga, Makamu Mwenyekiti Bara Isihaka Rashid Mchinjita, ambaye yeye atatembelea majimbo 21 katika Miķoa ya Dar es Salaam na Morogoro.
Amewataja wengine kuwa ni Katibu Mkuu wa chama hicho, Ado Shaibu yeye atatembelea majimbo 29 katika Mikoa ya Mtwara, Lindi, Pwani, Geita, Mwanza, Simiyu, Kagera na Mara na Kiongozi wa Chama hicho Mstaafu Zitto Kabwe atakuwa na ziara kwenye Majimbo 29 ya Mikoa ya Iringa, Njombe, Ruvuma, Mbeya na Songwe.
Shangwe ameeleza kuwa malengo ya awamu ya pili ya ziara hiyo ni kuendelea kuimarisha chama kilichoenea Tanzania Bara na Zanzibar katika kona zote za Tanzania. "Huu ni utekelezaji wa agizo la Halmashauri Kuu ya Chama kuwa kabla ya kampeni za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa ni lazima viongozi wakuu wa Chama wafanye ziara kwenye kila Jimbo katika Majimbo yote 214 ya Tanzania Bara. Ziara hii ya awamu ya pili inakamilisha utekelezaji wa agizo hilo." amesema Shangwe
Ameeleza engo la pili kuwa ni kukagua utekelezaji wa Azimio la Halmashauri Kuu ya Chama la kuhakikisha kila Kitongoji, Kijiji na Mtaa kina mgombea wa ACT Wazalendo kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
"Halmashauri Kuu ya Chama imeagiza Chama kisimamishe wagombea kwenye vitongoji, vijiji na mitaa yote nchini. Ziara hii inakwenda kuhakikisha hakuna kitongoji, kijiji wala mtaa wowote unakwenda kwenye uchaguzi ujao wa Serikali za
Mitaa bila kuwa na mgombea wa ACT Wazalendo." amesema na kuongeza kuwa;
"Wanachama 418,000 wameandaliwa kuwa wagombea katika ngazi mbalimbali zinazogombewa katika uchaguzi huu wa Serikali za Mitaa."
Ameendelea kueleza kuwa lengo lingine ni kuhamasisha kampeni ya Chama ya kusajili wanachama Milioni 10 kwa miezi 10 ambayo ilizinduliwa rasmi tarehe 22 Julai 2024. ACT Wazalendo imejiwekea lengo la kuwa Chama chenye idadi kubwa zaidi ya wanachama nchini ifikapo mwezi Aprili, 2024 na kusikiliza changamoto za wananchi na kuzitolea majawabu kwa kuzingatia ahadi ya ACT Wazalendo kwa Watanzania ya Taifa la Wote, Maslahi kwa Wote.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED