RIPOTI MAALUM: Uporaji simu, mikoba kwa bodaboda watisha

By Waandishi Wetu , Nipashe
Published at 06:44 AM Sep 08 2024
Uporaji simu, mikoba kwa bodaboda watisha
Picha:Nipashe Digital
Uporaji simu, mikoba kwa bodaboda watisha

HALI inatisha. Ndiyo hali halisi kutokana na wimbi la uporaji wa mikoba, simu na vitu vingine vya thamani unaofanywa na baadhi ya waendesha bodaboda kurejea kwa kasi katika miji mbalimbali, hivyo kuzua taharuki kwa wananchi.

Kwa wanaopora simu, wamekuwa wakituma ujumbe mfupi wa kuomba fedha za dharura kwa kutumia namba zilizoko katika siku iliyoibwa na baadhi bila kujua hulizwa.

Uchunguzi uliofanywa na Nipashe hivi karibuni katika maeneo mbalimbali nchini, umebaini matukio hayo hufanyika bila kujali ni mchana au usiku. Wengi  wanaoibiwa ni wale wanaotembea kwa miguu au wanaokuwa kwenye bodaboda au bajaji.

Wahalifu hao wamekuwa wakipakizana wawili katika bodaboda na abiria wake ndiye hutekeleza uporaji huo, huku baadhi ya wanaoibiwa wakiachwa na majeraha kutokana na kuvutwa kwa nguvu na ghafla.

WALIVYOLIZWA

Renatus Mahima, mkazi wa Kimara, Ubungo mkoani Dar es Salaam, anayefanya kazi kwenye kiwanda kimojawapo Mikocheni, anasilimulia kilichomsibu Agosti 24, mwaka huu.

“Nilitoka ofisini majira ya saa 1:00 usiku nikatembea mpaka Mwenge Mpakani, kiliko kituo cha daladala na bajaji, nilipofika pale nikachukua bajaji za kwenda Mbezi. Ndani ya bajaji tulikuwa abiria wanne, nilikuwa nimekaa siti ya nyuma na wanawake wawili, mimi nikiwa mlangoni na mbele alikuwako abiria mwingine mtu wa makamo.

“Nilitoa simu mfukoni ili kusoma ujumbe niliotumiwa kwenye simu. Tulipokaribia kituo cha Mlimani City ghafla ikatokea bodaboda nyuma ikiwa katika mwendokasi. Walikuwa  wamepakizana wawili, yule wa nyuma akavuta simu, wakanivuta na mimi nikaanguka kutoka katika bajaji,” anasimulia.

Mahima anasema bahati nzuri baada ya kudondoka nyuma hakukuwa na gari lakini  aliumia kwa kuchubuka mkono wa kulia na magoti yote.

“Dereva wa bajaji alinisubiri na ndiye aliyenisaidia simu yake nikapiga simu kampuni husika wakazima laini. Laini ya mtandao wa simu nyingine sikuizima kwa wakati ule mpaka nilipofika nyumbani kwa sababu sikupata mtu mwenye namba ya kampuni hiyo,” anasema.

Anasema saa moja na nusu baadaye alipotumia kompyuta mpakato kufuatilia simu yake, alibaini tayari iko maeneo ya Chamazi, Temeke mkoani Dar es Salaam. 

Hata hivyo, anasema hakutoa taarifa polisi wala Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), zaidi ya kufuta taarifa zake zote katika simu kwa kutumia kompyuta yake.

“Kuna namna ya kufuta taarifa zako kwenye simu kwa kutumia IMEI (International Mobile Equipment Identity) ya simu au gmail uliyokuwa unatumia kufungua mafaili kwenye simu,” anasema.

IMEI ni namba ambazo zinakuwa kama utambulisho wa kifaa na katika simu, mara nyingi zinakuwa na tarakimu 15 na huwa hazifanani zinakuwa katika kifaa kimoja tu. Pindi mtu akiibiwa kifaa au simu huwezesha kufuatilia nyendo za simu hiyo kama ikiwa imeunganishwa na intaneti na kuweza kufuta kila kitu na kuifunga kabisa simu hiyo kutumika tena kupitia IMEI ya simu hiyo.

Mkazi wa Mwenge, Dar es Salaam, ambaye hakutaka majina yake kuandikwa gazetini, anasimulia kuwa mwaka jana, aliibiwa simu yake majira ya asubuhi eneo la Sinza Mapambano, wakati akizungumza na mwendesha bodaboda wapi ampeleke.

“Wakati ninajiandaa kupanda huyo mtu wa bodaboda aliondoa ghafla bodaboda yake akiwa ameiba simu yangu na kuniacha. Muda mfupi mbele watu wangu wa karibu wakaanza  kutuma ujumbe wa kuombwa fedha kuanzia Sh. 200,000 hadi Sh. milioni moja na wapo waliotuma. 

“Kama hiyo haitoshi walichukua fedha kwenye akaunti Sh. milioni sita. Nilitoa taarifa polisi na kila nilipofuatilia nilikuwa ninaambiwa subiri mpaka nikaamua kuacha ,” anasema.

Akitaja namba walizotumia kuhamishia fedha hizo baada ya kufanya wizi kwenye akaunti yake alisema ni 0769860535, 0716986400 na 0699147562.

Mkazi wa Makumbusho, Dar es Salaam, Remi Kibago, anasema hivi karibuni ameshuhudia maeneo ya Mikocheni B, bodaboda wakikwapua pochi ya mwanamama  aliyekuwa amesimama pembezoni ya barabara kisha kuondoka nayo.

“Asilimia kubwa wenye tabia kama hizo hata mtaani wanajulikana. Kikubwa  Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na raia wema wafanye msako wa kuwatafuta vijana wote wanaojihusisha na vitendo hivyo,” anasema. 

Mariam Salehe, anasema mbinu ambazo wahalifu hao hutumia ni kuangalia eneo lenye upenyo mkubwa ili wasikamatwe.

“Baadhi wanatembea na panga wakiona hakuna watu wengi, dereva anasimama alafu abiria wake ambaye ni mhalifu mwenzake anashuka na kutumia panga kutishia ili utoe simu, fedha au chochote cha thamani kisha wanaondoka,” anasema.

 Mkazi wa Mtaa wa Bukoba, Manispaa ya Bukoba, mkoani Kagera, Hellen Joackim, anasema wizi unaohusisha waendesha bodaboda umekua kwa kasi hivi sasa.

 “Wizi huu unafanyika kwa njia tofauti, kwa kumkwapua mwenda kwa miguu alichonacho au wanapopakia abiria kukusafirisha sehemu moja kwenda nyingine njiani anaibiwa kila alichonacho kisha anatelekezwa,” anasema.

Mkazi wa Kata ya Miembeni, Aidan Heleman anasema: "Mei, mwaka huu, majira ya saa 5:00 usiku nilichukua bodaboda anipeleke nyumbani, ile tumefika nilipompa Sh. 5,000 ili akate Sh. 2,000 yake akatokomea na fedha yote.”

Mwendesha bodaboda wa mjini Bukoba, Josephat Katwale, anasema matukio hayo yako kwa vijana ambao sio waaminifu na hasa hutokea nyakati za usiku.

Jijini Arusha, baadhi ya wananchi akiwamo Andrew Daniel, wamesema matukio hayo yalipungua baada ya waliokuwa wakikamatwa kuchomwa moto, lakini hivi sasa yamerejea kutokana na wananchi kuacha kuchukua hatua mkononi.

Hamis Ramadhani, mwendesha bodaboda jijini humo, anasema, “Wizi unaofanywa na baadhi ya wanaotumia bodaboda, lawama hurudi kwetu wakati wengine hatuhusiki.”

Katibu wa Chama cha Waendesha Bodaboda mkoani Manyara, Athuman Shaban, anasema matukio ya wizi yalikuwapo kipindi cha nyuma ila kwa sasa yamedhibitiwa mkoani humo.

Mkoani Kilimanjaro, wizi wa kutumia bodaboda  unalalamikiwa zaidi kutikisa katika Manispaa ya Moshi na Wilaya ya Hai, ambapo mfanyabiashara Baraka Hussein, anasema huhusisha zaidi wizi wa simu, pochi na vitu vingine vya thamani kama cheni za dhahabu na za fedha.

Katika Mji wa Hai, Onesmo Kimaro, anasema upande wao baadhi ya bodaboda hutumika kubeba mifugo ya wizi kama nguruwe na mbuzi hasa nyakati za usiku.

WAJITETEA 

Dereva bodaboda wa eneo la Makumbusho, Rasul Musa, anasema wanaofanya matukio hayo si bodaboda waliosajiliwa bali ni wezi wanaotumia vyombo hivyo kuchafua tasnia hiyo.

“Haiwezekani kama kwa siku mtu unapata mpaka Sh. 30,000 kwa kubeba abiria halafu tena ushawishike kwenda kuiba kitu cha mtu. Haiingii akilini kabisa hao wanaofanya hivyo ni wezi," alisema. 

WATOA USHAURI 

Jabiri Mtumba, ameishauri serikali kuharakisha mpango wake wa ufungaji kamera za CCTV katika Barabara, ili iwe rahisi kubaini matukio ya uhalifu yanapotokea na wahusika kukamatwa.

Pia anasema kamera hizo zikiwamo maeneo mengine ya mtaani katika makazi ya watu zitasaidia kupunguza matukio hayo kwa sababu wataogopa kujulikana.

Gift Mtyauli, aliishauri serikali kuwasajili bodaboda kwa namba ili iwe rahisi kutambuliwa iwapo atafanya uhalifu.

Baadhi ya wakazi mkoani Kagera na Mwanza wameiomba serikali kuweka utaratibu maalum wa kuwatambua bodaboda wote nchini ili kudhibiti matukio hayo na mengine.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti wananchi hao akiwamo Vanessa Michael, mkazi wa Mwanza, anasema hatua hiyo ndio mwarobaini wa vitendo hivyo vinavyoendelea katika baadhi ya maeneo.

Akizungumza kwa niaba ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Ofisa Mnadhimu Kamishna Msaidizi (ACP) Yussuf Daniel, alikiri kupokea kesi za namna hiyo na wanaendelea na utaratibu kuona njia sahihi ya kuzikomesha.

Daniel aliwataka wananchi kutoa taarifa za wote ambao wanawatilia mashaka na kuwa na ushahidi wa kuhusika na matukio hayo ili waweze kuyakomesha.

Alipotafutwa Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano kwa Umma wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Rolf Kibaja, alisema anafahamu kuwapo kwa matukio hayo lakini vitendo hivyo hushughulikiwa na Jeshi la Polisi.

“Huwa tunapokea malalamiko kwa watu mbalimbali kuhusu kuibiwa simu, lakini sehemu sahihi kwa malalamiko yao ni polisi kwa sababu wao ndio wanahusika na wizi wa aina yoyote ile, hata huu wa simu kwa sababu inaonekana wakishapora tena wanaanza kutapeli watu.

“Masuala yote ya utapeli na uhalifu, mamlaka husika ni Jeshi la Polisi japo huwa tunapokea malalamiko kutoka kwa wateja na huwa tunawaelekeza sehemu husika kwa ajili ya hatua za kipolisi,” alisema.

Hata hivyo, Nipashe ilipomtafuta Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, Naibu Kamishna (DCP) David Misime, kwa kumwandikia maswali katika WhatsApp yake alisoma, lakini hakujibu na alipopigiwa hakupokea.