DMDP II kujenga Kilomita 250 za lami

By Mary Geofrey , Nipashe
Published at 04:54 PM Oct 24 2024
DMDP II kujenga Kilomita 250 za lami
Picha:Mpigapicha Wetu
DMDP II kujenga Kilomita 250 za lami

Serikali imetia saini mikataba ya Ujenzi wa Barabara katika Halmashauri tano za Mkoa wa Dar es Salaam kupitia Mradi wa Uendelezaji wa jiji hilo, Awamu ya Pili(DMDP II) utakaojenga Kilometa 250 za kiwango lami.

Utekelezaji wa mradi huo, utaanza Desemba mwaka huu na jumla ya huo utajenga na kuboresha Kilomita 90 za mifereji ya maji na kujenga vituo vya mabasi  tisa, masoko 18 na madampo matatu ya kisasa.

Mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA) Mhandisi Humfrey Konyenye, ameyasema hayo leo mbele ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mohamed Mchengerwa wakati wa hafla hiyo.

Amesema kuwa jumla ya kata 72 na wananchi milioni 4 wa mkoa huo watanufaika na mradi huo.

Amesema gharama za mradi huo ni Dola za Marekani milioni 438  sawa na zaidi ya Sh. Trilioni moja.

"Kati ya fedha hizi, Benki Kuu imetoa Dola milioni 385 na Serikali ya Uholanzi, itatoa ruzuku ya Dola za Marekani milioni 53," amesema Konyenye.

Awamu ya kwanza ya DMDP, ilijenga na kuboresha Kilomita 207 za barabara za lami katika Manispaa ya Temeke, Ilala na Kinondoni.