UCHAGUZI UJAO: CHADEMA yaguna uandikishaji wapigakura wa Serikali za Mitaa

By Mussa Mwangoka , Nipashe
Published at 10:56 AM Oct 24 2024
CHADEMA yaguna uandikishaji   wapigakura wa Serikali za Mitaa
Picha: Nipashe Digital
CHADEMA yaguna uandikishaji wapigakura wa Serikali za Mitaa

UONGOZI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) mkoani Katavi umekosoa uandikishaji wapigakura wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, ukidai kuwa uligubikwa na dosari nyingi.

Umesema dosari hizo hazipaswi kujirudia katika hatua nyingine za mchakato wa uchaguzi huo kwa kuwa zinatia doa uchaguzi huo na mustakabali wa demokrasia nchini.

Mwenyekiti wa CHADEMA Mkoa wa Katavi, Rhoda Kunchela, alitoa rai hiyo jana wakati akizungumzia mchakato wa uchaguzi huo uliopangwa kufanywa Novemba 27, mwaka huu.

"Kuna kasoro nyingi: Majina kuandikwa kwenye makaratasi ya kawaida, si kwenye daftari la Tume Huru ya Uchaguzi; wanafunzi wasio wakazi wa eneo husika kuandikishwa, pia watoto chini ya miaka 18 kuandikisha kupiga kura na mengine mengi ambayo tumeainisha na kuitaka Tume ya Uchaguzi ishughulikie ili isitie doa uchaguzi huo," alisema.

Hata hivyo, uchaguzi huo unasimamiwa na Ofisi ya Rais - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) licha ya marekebisho ya kisheria kuelekeza usimamiwe na Tume Huru ya Uchaguzi (INEC). 

Alisema hawategemei hatua zinazofuata kwenye mchakato huo ziwe na malalamiko, hivyo mamlaka inayousimamia itende haki kuanzia kwenye uchukuaji fomu na inapofika hatua ya mapingamizi, haki pia itendeke, vivyo hivyo wakati wa kampeni hadi siku ya upigaji kura.

Rhoda ambaye amewahi kuwa mbunge wa viti maalumu mkoa huo, alisema CHADEMA imewashawishi wananchi kujitokeza kujiandikisha kwa kuwa wengi wao walionesha kukata tamaa kutokana na kila mara kuporwa haki yao.

Hivyo, wana matumaini uchaguzi huo utatoa taswira ya nini wanatakiwa kufanya kwenye Uchaguzi Mkuu ujao  wa rais, wabunge na madiwani.

Kwa mujibu wa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais - TAMISEMI, Mohamed Nchengerwa, wananchi waliojiandikisha kupiga kura kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa Novemba 27, mwaka huu mkoani Katavi ni asilimia 96.37 ya waliotarajiwa kuandikishwa katika mkoa huo.

Oktoba 21 mwaka huu, wakati akifunga uandikishaji wapigakura kwa ajili ya uchaguzi huo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais - TAMISEMI, Mohamed Mchengerwa, alivitaka vyombo vya dola nchini kuhakikisha vinaimarisha usalama ili uchaguzi huo uwe wa huru na haki.

Alipoulizwa kuhusu malalamiko ya vyama vya siasa, ikiwamo CHADEMA, kwamba baadhi ya wanafunzi wameandikishwa kupiga kura, Waziri Mchengerwa alisema, hoja hiyo haina mashiko "kwa sababu katika shule wapo pia wanafunzi waliozidi umri wa miaka 18 ambao sifa zinawaruhusu kupiga kura".

Alipoulizwa kuhusu malalamiko ya CHADEMA na ACT Wazalendo kuhusu eneo la Mirerani, mkoani Manyara kwamba uandikishaji ulifanyika hadi usiku, waziri huyo alisema "sina malalamiko hayo na sifahamu chochote. Kama tungepata taarifa hiyo, tungeifanyia kazi, tunataka uchaguzi wa huru na wa haki."

Kwa mujibu wa Waziri Mchengerwa, jumla ya wapigakura 31,282,331 wameandikisha kwa ajili ya uchaguzi huo sawa na asilimia 94.83 ya lengo la kuandikisha watu 32,897,8579.