Waliomteka Tarimo walitaka kumlawiti

By Grace Gurisha , Nipashe
Published at 08:39 PM Feb 12 2025
Tukio la utekaji la Mfanyabiashara Deogratus Tarimo.
Picha:Mtandao
Tukio la utekaji la Mfanyabiashara Deogratus Tarimo.

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kinondoni imeelezwa kuwa vijana sita, wakiwemo mabondia wawili, walipanga kumteka mfanyabiashara Deogratus Tarimo kwa lengo la kumlawiti na kumsababishia maumivu.

Kesi hiyo, inayowakabili washtakiwa Fredrick Nsato (21), bondia Isaack Mwaifuani (29), Benk Mwakalebela (40), bondia Bato Twelve (32), dereva teksi Nelson Msela (24), na Anitha Temba (27) maarufu kama Jack, imeendelea kusikilizwa mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Ramadhani Rugemalira.

Wakili wa Serikali Mkuu, Nassoro Katuga, amesema kuwa Anitha alihusika katika kumshawishi Tarimo kukutana naye hotelini kwa madai ya kujadili biashara, ambapo alinaswa kwenye mtego wa washitakiwa waliokuwa na mpango wa utekaji.

Ilidaiwa kuwa Novemba 11, 2024, Tarimo alipofika hotelini, Anitha alimwelekeza kusubiri katika kaunta ya baa. Baada ya muda mfupi, washtakiwa Mwaifuani, Mwakalebela, na Twelve waliwasili katika gari aina ya Toyota Raum namba T 237 EGE na kujitambulisha kama polisi.

Walipomvuta Tarimo kuelekea kwenye gari, alipiga kelele, hali iliyowafanya kumwachia na kumtishia kuwa wangempata tena. Taarifa zilifikishwa katika Kituo cha Polisi Gogoni na uchunguzi ukaanza, hatimaye kusababisha kukamatwa kwa washitakiwa hao.

Washtakiwa walikana mashtaka dhidi yao huku Anitha akikataa jina lake maarufu la Jack. Mahakama ilikubali ombi la kubadilisha shtaka kutoka "jaribio la utekaji" hadi "utekaji nyara" baada ya ushahidi mpya kuwasilishwa.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Februari 24, 2025, kwa ajili ya kusikilizwa zaidi.