Biteko aita wawekezaji nishati kuja nchini

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 06:12 PM Feb 12 2025
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko akizungumza kwenye
Mkutano wa Mawaziri wa Nishati kutoka India, Sudan, Malawi, Rwanda, Nepal, Brazil.
Mkutano huo umefanyika leo Februari 12, 2025 jijini New Delhi nchini India
Picha: Mpigapicha Wetu
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko akizungumza kwenye Mkutano wa Mawaziri wa Nishati kutoka India, Sudan, Malawi, Rwanda, Nepal, Brazil. Mkutano huo umefanyika leo Februari 12, 2025 jijini New Delhi nchini India

NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko, amewakaribisha wawekezaji kutoka nchi mbalimbali duniani, kuwekeza katika sekta ya nishati nchini.

Akizungumza leo, Februari 12, 2025,  jijini New Delhi, India, katika Mkutano wa Mawaziri wa Nishati kutoka India, Sudan, Malawi, Rwanda, Nepal, Brazil pamoja na wakurugenzi wa kampuni mbalimbali, Dk. Biteko amesema serikali imeweka mazingira wezeshi, ili kuhakikisha kuwa Nishati Safi ya Kupikia, inapatikana kwa urahisi na gharama nafuu.

Amesema mwaka 2022, serikali ilisisitiza matumizi ya nishati safi na kueleza athari za matumizi ya nishati isiyokuwa safi, kwa kuanzisha mjadala wa kwanza ambao uliongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan.

Dk. Biteko ametaja fursa mbalimbali za biashara ya Nishati Safi ya Kupikia nchini Tanzania, kama vile ujenzi wa miundombinu ya uzalishaji, kupokea, kuhifadhi na kusambaza nishati safi ya kupikia

Mawaziri wa Nishati kutoka India, Sudan, Malawi, Rwanda, Nepal, Brazil wakiwa kwenye Mkutano wa Mawaziri wa Nishati uliofanyika leo Februari 12, 2025 jijini New Delhi nchini India ikiwa ni sehemu Wiki ya Nishati India
Fursa zingine, amezitaja kuwa ni vituo vya kupokea LPG, vifaa vya uhifadhi, miundombinu ya usambazaji wa gesi asilia katika mikoa ya Mtwara, Lindi, Pwani, Dar es Salaam na maeneo jirani, usambazaji wa LNG wa kiwango kidogo, vifaa na mitungi ya gesi asilia.

“Hivyo basi, ningependa kuchukua fursa hii, kuwataka wadau wote na wawekezaji katika sekta ya nishati kujiunga nasi katika malengo yetu makubwa, lakini yanayoweza kufikiwa ya kupata umeme na Nishati Safi ya kupikia.

“Kuongeza sehemu ya nishati mbadala katika mchanganyiko wa nishati na kuongeza uwekezaji wa sekta binafsi, ili kusaidia upatikaji wa nishati,” amesema Dk. Biteko.

Hata hivyo, ametaja jitihada za serikali za kuhamasisha matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia “Tanzania imekamilisha maendeleo ya Mkakati wa Kitaifa wa Nishati Safi ya Kupikia kwa mwaka 2024-2034, wenye lengo kuu la kuhakikisha kuwa asilimia 80 ya Watanzania wanatumia Nishati Safi ya Kupikia ifikapo mwaka 2034,.”

Ameongeza: “Katika kujifunza kutokana na uzoefu wa nchi zingine tumegundua kuwa India imefanya vizuri  kwani takwimu zinaonyesha kwamba  mwaka 2023, asilimia 71.1 ya watu wa India, walikuwa wakitumia nishati safi ya kupikia. 

“Hii imetokana na umuhimu wa kuhusisha sekta binafsi na kuunganishwa kwa ruzuku kwa kaya zenye kipato cha chini,”

Katika hatua nyingine, Dk. Biteko amesema: “Kulingana na takwimu, takriban watu bilioni 2.3 duniani hawapati nishati safi ya kupikia na watu milioni 990 katika Sub-Sahara Afrika, hawafikiwi na nishati safi. Hali hii inasababisha matatizo ya afya, uharibufu wa mazingira na matatizo ya kiuchumi,”

Vilevile, amesema Rais Samia amedhamiria kuipeleka ajenda ya nishati safi ya kupikia nje ya mipaka ya Tanzania na Afrika na katika mkutano wa COP 28, alizindua Programu ya Uwezeshaji wa Nishati Safi ya Kupikia kwa Wanawake wa Afrika (AWCCSP), iliyoelekezwa kukabiliana na changamoto kubwa za kijinsia, mazingira, afya, na kiuchumi zinazowakabili wanawake na wasichana barani humo.

Akiendelea kuelezea msimamo wa Tanzania katika kuhamasisha Ajenda ya Matumizi ya Nishati Safi kimataifa, Dk. Biteko amesema mwaka 2024, Rais Samia alishiriki katika Mkutano wa Juu wa Nishati  Safi ya Kupikia Ufaransa na alihudumu kama mwenyekiti mwenza na takriban dola bilioni 2.2 ziliahidiwa, kwa ajili kusaidia ajenda hiyo.

Aidha, Tanzania kwa kushirikiana na Tume ya Nishati ya Afrika (AFREC), ilifanya Mkutano wa Kiwango cha Juu kuhusu Kupikia Nishati Safi barani Afrika katika Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Septemba 2024, pamoja na kuwa mwenyeji wa Mkutano wa Nishati wa Wakuu wa Nchi za Afrika uliyofanyika jijini Dar es salaam Februari  27 na 28, mwaka huu, kwa ajili ya kueleza dhamira zao juu ya utekelezaji wa Mikataba ya Nishati ya Kitaifa.

Waziri wa Petroli na Gesi Asilia wa India, Hardeep Singh, ametaja madhara ya matumizi ya nishati isiyosafi.

“Kumekuwapo na idadi ya vifo takribani milioni mbili, lakini wanawake na watoto wanapata madhara zaidi, huku wanawake wakitumia hadi saa 5 kila siku kwa ajili ya kutafuta kuni na kuandaa chakula.”

Akielezea mafanikio ya matumizi ya nishati safi nchini India, amesema sasa watu milioni 330 wameunganishwa na matumizi ya nishati safi.

 “Nishati safi sasa inapatikana kwa watu na maisha yamekuwa rahisi na shughuli zimeendelea kufanyika kwa ufanisi, sioni kwa nini hatuwezi kufanya hivi kwa kila mwananchi  inawezekana.”