BINGWA wa masuala ya utengemao amebainisha kuwa, watoto wanaozaliwa wakiwa na changamoto ya mtindio wa ubongo haina maana kwamba wana tatizo la akili, badala yake tatizo pekee linalowakabili ni kushindwa kumudu vizuri kutembea.
Msingi wa kauli hiyo umetokana na kuwepo kwa kasumba kwa baadhi ya watu kuwachukulia watoto wenye tatizo hilo linalotambulika kitaalamu kama ‘Cerebral Palsy’ (CP), kuwa hawana uelewa wala uwezo wa kiufahamu jambo ambalo sio sahihi.
Akizungumza na Nipashe siku chache zilizopita bingwa huyo ambaye ni Mkuu wa Idara ya Utengemao katika hospitali ya CCBRT, Dk. Ruth Onesmo, alisema wenye tatizo la mtindio wa ubongo wakifundishwa wanasikia na kuelewa na ukuaji wa ufahamu wao uko vizuri.
“Ugonjwa wa utindio wa ubongo unaathiri zaidi utembeaji kutokana na athari iliyojitokeza kwenye ubongo, lakini sio ufahamu wa mtoto, wako ambao tunawahudumia katika Shule ya Jangwani na Pugu Sekondari na wanafanya vizuri,” alisema na kuongeza;
“Tunaweza kupata watoto wenye utindio wa ubongo sio kwasababu hatujawatunza wakiwa tumboni au kuna mtu ametuloga, ama hatuna bahati. Tatizo hilo linaweza kutokea wakati wa mtoto kuzaliwa endapo atabanwa kichwani, lakini pia unaweza kusababishwa na homa ya manjano inayosababisha mtoto kukosa kunyonya kwa muda mrefu, pamoja na kuangushwa,” alisema Dk. Ruth.
Alieleza kuwa katika idara yao ya utengemao ambayo ni mahususi kwaajili ya kuwahudumia watoto wenye tatizo hilo, mwaka 2024 walitoa huduma za tiba kwa vitendo kwa watoto 6,508, vifaa tiba saidizi ya 1,686 ikiwemo viti mwendo, na kuwatembelea watoto wenye changamoto na kuhakiki miundombini rafiki katika mazingira yanayowazunguka.
Alieleza kuwa wamewaelimisha wazazi pia namna ya kuwahudumia watoto hao, pamoja na kuwaongezea uwezo wa uelewa baadhi ya wataalamu wa afya wasiojua kuwa CP inatokana na nini na namna ya kuwahudumia wagonjwa wenye tatizo hilo kwa usahihi.
Hata hivyo, alieleza kuwa mwaka huu wanalenga kutoa huduma ya tiba kwa vitendo kwa watoto 1,000 na kuwasaidi wengine viti mwendo 200, pamoja na vifaa tiba vingine vyote watakavyokuwa na uhitaji navyo, akisisitiza kwamba endapo wenye tatizo hilo watapatiwa matibabu stahiki wanauwezo wa kurudi katika hali yao ya kawaida.
Alieleza kuwa wanatarajia pia kuboresha au kununua vifaa vingine mbalimbali vya kisasa kwaajili ya kutolea huduma hiyo ya utengemao kwa watoto wenye changamoto ya utindio wa ubongo kote nchini, na kwamba jitihada hizo zinaungwa mkono wa wadau mbalimbali wa afya na maendeleo.
“Kwa kushirikiana na serikali na wadau mbalimbali wa maendeleo CCBRT imefanikiwa kutoa huduma ya matibabu kwa watu zaidi ya milioni moja tangu kuanzishwa kwake mwaka 1994, na tumeendelea kuwapatia huduma bure wale wote wanaopata mimba wakiwa chini ya miaka 18,” alisema Dk. Ruth.
Pia alisema wanatoa pia huduma za utengemao bila malipo kwa Mama wenye historia ya kupata fistula, waliopata watoto wenye ulemavu na kuathirika kisaikolojia, pamoja na wale waliozaliwa na mdomo sungura.
“Nitoe wito kwa watanzania kushirikiana kwa pamoja katika jitihada za kuwasaidia na kuwawezesha watoto hawa waweze kupata matibabu na kutimiza ndoto zao,” alisema Dk. Ruth.
Kadhalika, inaelezwa kuwa CP inatokana na uharibifu wa sehemu za ubongo zinazodhibiti shughuli za misuli. Na kwamba utindio wa ubongo unaweza kutokea wakati wa ujauzito, wakati wa kuzaliwa, baada ya kuzaliwa, au katika utoto wa mapema, ikielezwa kuwa athari zinaweza kuonekana zaidi endapo mtoto atazidi kukuwa bila kupata tiba stahiki.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED