DIWANI wa Kata ya Ibadakuli Manispaa ya Shinyanga Msabila Malale, na diwani wa Vitimaalumu wa Kata hiyo Zuhura Waziri,wamedaiwa kupigana makonde kwenye zoezi la kura za maoni ndani ya chama cha mapinduzi (CCM) la kuwachagua wagombea ambao watapeperusha bendera ya chama hicho kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa.
Tukio hilo limetokea jana kwenye Kata hiyo ya Ibadakuli, wakati zoezi hilo likiendelea la upigaji wa kura za maoni la kuwapata wagombea wa CCM, ambao watawania nafasi za uongozi kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika novemba 27 mwaka huu.
Diwani Msabila akielezea tukio , amesema wakati wagombea walivyomaliza kujinadi, na wajumbe kuanza kupewa karatasi za kupiga kura, alihoji "Mbona kwenye mfuko wa kuweka kura zilizopigwa hamjajiridhisha kama kuna usalama,?"
Amesema baada ya mfuko kukung'utwa ilianguka kura moja ambayo ilishapigwa kisha hakamuona tena msimamizi akiwapigia kura watu wasiojua kusoma na kuandika.
"Ndipo nilihoji kisha Diwani wa Vitimaalumu, Zuhura Waziri, ambaye ndiye alikuwa msimamizi mkuu wa uchaguzi huo akaniambia nisiwafundishe kazi alafu akanisusia bahasha za karatasi za upigaji kura"
Amefafanua kwamba diwani huyo (Zuhura) alianza kumtolea maneno ya kashfa, na kwamba wao ndiyo wamechaguliwa kusimamia uchaguzi huo, yeye diwani (Msabila) amekwenda kufanya nini hapo bali anapaswa kuondoka.
Msabila amesema alimjibu hapo ni kituo chake cha kupiga kura, na kwamba baada ya muda diwani huyo (Zuhura) akiwa na Katibu Mwenezi wa Kata ya Ibadakuli na wajumbe wengine, walikaa pembeni wakiongea, lakini gafla Zuhura alimsogelea na kuanza kumwambia hamjui,huku na yeye akijibu kwamba hamjui ndipo ugomvi ukaanza.
“Zuhura yeye alinirukia ili kunikamata sehemu zangu nyeti, na mimi nikamkamata kumtoa wala siku mpiga, ndipo watu wakajaa na kutuamua ndivyo ilivyokuwa Mwandishi,” amesema Msaliba.
Naye Diwani wa Vitimaalumu Zuhura Waziri,alipopigwa na Nipashe kujua hali ilivyokuwa,amesema hawezi kuzungumzia suala hilo kwa sasa, kwa kuwa anajisikia vibaya baada ya kudai kupigwa na diwani huyo.
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini Anold Makombe, amesema taarifa za tukio la madiwani hao kupigana bado hajazipata vizuri, na akizipata taarifa zaidi atalizungumzia kwa kuwa muda huo anaelekea kwenye kikao ofisi za CCM.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED