Fursa za Mbaazi na faida zake kiafya

By Maulid Mmbaga , Nipashe
Published at 02:54 PM Oct 24 2024
Mbaazi.
Picha: Maulid Mmbaga
Mbaazi.

MBAAZI ni miongoni mwa mazao ya jamii ya mikunde ambalo miaka ya karibuni lilisahaulika na kupewa kisogo nchini hali ambayo imewafanya wadau wa maendeleo nchini kuliwekea mikakati ya kulirudisha sokoni, baada ya kubaini faida zake kiafya na kijamii.

Inaelezwa kuwa Mbaazi sio zao ambalo lilikuwa likipewa kipaumbele zaidi nchini tofauti na mataifa mengine ambako kwa kiasi kikubwa kiwango kilichokuwa kikizalishwa kilikuwa kinasafirishwa kwenda mataifa ya nje kama India. 

Kutokana na umuhimu wake katika lishe, wadau wa maendeleo kama Taasisi ya Uendeshaji wa Mifumo ya Masoko ya Kilimo (AMDT) wameweka mikakati madhubuti ya kuzalisha kwa wingi na kuwawezesha wakulima kupata mbegu bora zinazoendana na mabadiliko ya tabianchi.

Aidha, katika kutekeleza adhima hiyo AMDT imekuja na Mradi wa Maono ya Mabadiliko kwenye Mazao na Udongo (VACS) unaojumuisha utoaji wa elimu kuhusu kilimo cha umwagiliaji kwa njia ya matone, mfumo unaosaidia kuongeza uzalishaji na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Chini ya uratibu wa AMDT siku chache zilizopita Nipashe ilifika mikoa ya Arusha, Dodoma, Kilimanjaro na Manyara ili kujionea maendeleo ya utekelezaji wa mradi huo ambao kwa awahi hii umeelekezwa hasa katika mikoa hiyo.

MIKAKATI ILIYOKO

Mratibu wa tathmini na ufuatiliaji wa matokeo kutoka AMDT, Delta Shila, anasema taasisi hiyo imekuja na mkakati wa kuhamasisha ulaji wa Mbaazi, huku kipaumbele kikiwa ni kuona jamii inatambua umuhimu wa zao hilo hasa katika mlo wa kila siku.

Anasema wanachokifanya ni kuangalia namna gani wanajibu matakwa ya serikali ambayo moja kwa moja yanawalenga watanzania, na kwamba wameka jitihada za kurudisha thamani ya zao la Mbaazi kwa kuzijengea uwezo taasisi zinazofundisha mapishi katika kuboresha mapishi mbalimbali ya kutumia zao hilo.

“Bei ilidorora sana, tulikuwa tunategemea masoko ya nje na baada ya kwenda vibaya mwisho wa siku wakulima waliumia licha ya kwamba bado ni wadogo.

“kwahiyo pamoja na kuhamasisha kuuza Mbaazi nje ya nchi tumekimbizana sana kufanya kazi kwa karibu na taasisi mbalimbali katika kuongeza ulaji wa zao hilo,” anasema Shila.

Anasema wanaangalia ni namna gani wanaboresha na kuhakikisha watu wanafundishwa namna ya kutengeneza Mbaazi kwa milo tofauti ili kutengeneza soko la ndani, kwakuwa wamezoea kuona zinapelekwa katika mataifa mengine.

Wakulima wanaojihusisha na kilimo cha Mbaazi katika kijiji cha Seluka, Kata ya Chipogolo, Wilaya ya Mpwapwa mkoani Dodoma, wakiendelea na shughuli zao za kawaida katika shamba lenye ukubwa wa ekari 90 ambalo wameotesha zao hilo. PICHA: MAULID MMBAGA.
Pia anasema wanaendelea kujenga uwezo kwa wakulima kuzalisha mazao hayo na kuyapeleka kwa jamii ili kuhakikisha kwamba soko la ndani linaendelea kujiridhisha na mazao yanajisimamia yenyewe.

“Tunaangalia masuala ya mifumo ya kimasoko inakoanzia kwenye mbegu inaendaje shambani, mbolea inamfikiaje mkulima, pembejeo zake na masuala ya mikopo, lakini mwisho wa siku inarudije kwa watumiaji ili mkulima apate tija mfukoni mwake katika kujibadilisha kiuchumi,” anasema Shila.

Anasema wanashirikiana pia na Taasisi ya mbegu ya Beula kuhakikisha kwamba wakulima wanazalisha mbegu bora za Mbaazi, pamoja na lishe.

Anabainisha kuwa wanaendelea na mkakati wa kuishauri serikali iingize zao la Mbaazi katika mitaala ya ufundishaji mashuleni, pamoja na kushiriki vikao vya wazazi vya bodi kwenye mashule ili kuwahamasisha kutumia zao hilo na mengine ambayo ni jamii ya mikunde.

“Katika shule zetu za kata, mfano kuna maeneo ambayo wazazi wanapeleka kiasi kidogo cha chakula shuleni kwaajili ya mtoto kula, sasa hawezi kuamka tu na kupeleka Mbaazi wakati wenzake wamepeleka Maharage, tunachokifanya ni kuzifanya shule ziwe na uwezo wa kuwaambia wazazi kwamba wanaweza kuleta Mbaazi, Choroko au Kunde,” anasema Shila.

Anaeleza kuwa katika masoko wanamiradi ambayo inafanyika katika sula la kuongeza tija ili wakulima watakapozalisha wapate pa kuuza pia.

KUHUSU MBAAZI

Wakielezea zao hilo wanasema ni mmea jamii ya mikunde unaokuzwa sana katika maeneo ya tropiki na nusu tropiki. Na kwamba nchini Tanzania inalimwa kwa wingi katika mikoa ya kanda ya Kasklazini, Kusini na kanda ya kati.

Inaelezwa kuwa zao hilo ni maarufu sana katika jamiii na hutumika kama mboga ama chakula hasa kwa watu wa Pwani.

Inabainishwa kuwa Mbaazi ni mbegu yenye virutubisho vyenye protini, vitamin B, madini muhimu kwa binadamu kama ya chuma, Zinki na Kalisiam.

Hata hivyo, inaelezwa kuwa maeneo mengi hulima Mbaazi lakini watu hawapendelei kula zao hilo, huku utafiti ukionyesha kwamba watu wengi hawali Mbaazi kwasababu hawana elimu juu ya zao hilo hasa manufaa ya kilishe.

Sababu nyingine ilielezwa kuwa watu wengi hawafahamu mapishi mbalimbali ya Mbaazi, huku ikibainishwa kuwa kwa wale watakaotumia vyakula vinavyotakana na zao hili itawasaidia kuboresha afya zao, pamoja na kuinua uchumi wa wale wanaofanya biashara ya chakula.

Inaelezwa kuwa Mbaazi pia hutumika katika kutengeneza vyakula mbalimbali kama mkate, chapati za aina zote, skonzi, sambusa, kababu, keki, maandazi, donate, half keki, uji, supu, futari, na pia zinaweza kuchanganywa katika biriyani, na kande.
Mbaazi.

FAIDA KIAFYA

Ofisa Lishe kutoka Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) Dk. Husna Faraji, anasema kwenye gramu 100g za Mbaazi asilimia 60 ni makapi ambayo husaidia mtu katika matatizo ya kukosa choo na gasi, lakini pia kulinda afya ya moyo kwa kupunguza cholesterol.

Anasema Mbaazi husaidia kwenye afya ya mfumo wa chakula na kulinda moyo. Na kwamba zina madini ya potassium, fibers, magnesium na kiwango kidogo cha cholesterol, hivyo kudhibiti presha na cholesterol ambayo hupunguza hatari ya kupata magonjwa ya mishipa ya damu na moyo.

Pia anasema kwenye gram 100 ya Mbaazi kuna 22g ya Protini ambayo ni muhimu kwa ukuaji hasa wa watoto ambao wanaitaji sana Protini kwenye milo yao katika kupunguza utapiamlo, akieleza kuwa husaidia pia kutengenezwa kwa seli mpya za mwili, misuli, mifupa na kuweka msawazo wa sukari kwenye damu.

“Mbaazi inaweza kutumika kupungua uzito kutokana na kiwango kidogo cha calories, saturated fats na cholesterol, uwepo wa fibers nyingi ndio sababu kuu ya kukufanya upungue uzito. Husaidia kupungua uzito kutokana na uwepo wa dietary fibers (makapi mlo) kwa kiasi kikubwa ambazo humfanya mtu kuhisi ameshiba kwa mda na kuondoa hamu ya kula mara kwa mara,” anasema Dk. Husna.

Faida nyingine ni kusaidia kwenye mmeng’enyo wa chakula, kuzuia athari za kupatwa na magonjwa yasiyoambukiza mfano kansa, kisukari na ugonjwa wa moyo.

Nyingine ni kuweka msawazo wa homoni kwenye damu hivyo kusaidia kuzuia tatizo la homoni. Huku ikielezwa kwamba kwenye Mbaazi kunapatikana vitamini A, C, E na K.

Vile vile, wataalamu wa afya wanaeleza kuwa viini lishe vinavyopatokana kwenye Mbaazi zenye gramu 100 ni pamoja na nishati, mafuta, maji, Kabohaidreti, sukari, nyizilishe, na Protini.

UHITAJI

Mkurugenzi wa AMDT Charles Ogutu, anasema baada ya kuweka mikakati mbalimbali ya kuongeza tija ya zao la Mbaazi, kwa sasa wameanza kuona matumizi yake na bei imepanda kuliko walivyokuwa wanatarajia kwasababu virutubisho vyake ni vingi kuliko Maharage.

“Tumetoa kipaumbele kwenye mazao hayo hususani Mbaazi kutokana na manufaa yake kiafya na uhitaji wake katika jamii na kuna wawekezaji wanahitaji, pia tumehamashisha uzalishaji wake kwasababu tunaangalia mkulima azalishe kitu ambacho kitakuwa na soko,” anasema Ogutu.

Ofisa Uzalishaji wa Kampuni ya Mbegu ya Beula, Ernei Chiwele, anasema wanashirikiana na AMDT kusambaza mbegu bora ikiwemo ya Mbaazi kwenda kwa wakulima, na kwamba wameanzisha mashamba darasa kwa lengo la kuoaelimu kwa wakulima ili wawe na uelewa na kufanya uzalishaji wenye tija.