Tanzania yang’ara Afrika ufuatiliaji maafa

By Maulid Mmbaga , Nipashe
Published at 08:12 PM Oct 24 2024
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Dk. Jim Yonazi akiwasilisha mada kuhusu masuala ya menejimenti ya maafa Tanzania
Picha:Mpigapicha Wetu
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Dk. Jim Yonazi akiwasilisha mada kuhusu masuala ya menejimenti ya maafa Tanzania

TANZANIA imetajwa kuwa nchi ya kwanza barani Afrika kuwa na kituo cha ufuatiliaji wa mwenendo wa majanga na tahadhari ya mapema ambacho kimelifanya taifa kuwa kinara kwenye masuala ya menejimenti ya maafa hususani katika kuzuia, kupunguza kujiandaa na kukabili maafa pindi yanapotokea.

Kituo hicho cha Taifa cha Operesheni na Mawasiliano ya Dharura, ambacho kimetambulika kimataifa, pia kimeendelea kutumika kufanya ufuatiliaji wa uwezekano wa kutokea majanga kwa kutumia mifumo ya kiteknolojia ya kijiografia kwenye tamataizo yanayotokana na hali ya hewa na haidrolojia kwa kutumia jukwaa la kielektroniki la (MyDEWETRA).

Hayo yamebainishwa jana na Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu Dk. Jim Yonazi, wakati akiwasilisha mada katika kikao cha tisa cha Jukwaa la Kanda la Afrika linalohusiaka katika kupunguza madhara ya maafa, ambacho kimefanyika Namibia.

“Mfumo huu umerahisisha ufuatiliaji wa mwenendo wa janga lililotabiriwa na kufanya uchambuzi wa kiwango cha madhara kwa jamii, miundombinu na mazingira, kuandaa taarifa za tahadhari ya mapema ya hatua za kuchukua ili kuzuia, kujiandaa na kukabili maafa.

“Pia kuandaa taarifa ya mwenendo wa tukio na kusambaza kwa wadau mbalimbali kwa ajili ya kusaidia uratibu na utekelezaji wa shughuli za kukabili na kurejesha hali ya kawaida katika jamii,” amesema Dk. Yonazi.

Ameongeza kuwa uwepo wa kituo hicho cha ufuatiliaji wa majanga na tahadhari ya mapema umesaidia Tanzania kuendelea kuwa mstari wa mbele katika kukabiliana na maafa kabla hayajaleta madhara.

Pia amesema uanzishwaji wa kituo hicho umefanikiwa kutokana na mradi ulioanzishwa na Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kupunguza Madhara ya Maafa katika Kanda ya Afrika na kufadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Italia katika kusaidia kutoa utaalam wa utekelezaji wa shughuli zote.

Hata hivyo, Dk. Yonazi ametoa wito kwa  nchi  wanachama  pamoja na  mataifa mengine kuja Tanzania kwa lengo la  kujifunza na kubadilishana uzoefu kwa kuzingatia umuhimu wa ufuatiliaji na uzuiaji wa majamba ambayo yasipodhibitiwa husababisha madhara katika jamii.

Tanzania ni miongoni mwa nchi zilizoshiriki katika Kikao hicho cha siku nne ambacho kilianza Oktoba 21 na kumalizika   jana, na kwamba kiliwakutanisha wadau wa maafa wa nchi za Afrika zaidi ya 1,000 wakiwemo wataalamu kutoka katika ngazi za kitaifa, serikali za mitaa, mashirika ya umoja wa kitaifa na kimataifa, asasi za kiraia, sekta binafsi, taasisi za elimu na utafiti.