WAKATI Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) kikitarajia kusherehekea miaka 60 ya chuo hicho uongozi wa chuo hicho umesema unatarajia kuhakikisha wanafunzi wenye vipaji wanafika mbali kwa kuwa maono yao ndiyo mafanikio yao.
Hayo yalisemwa jana na Mkuu wa chuo hicho, Profesa Edda Lwoga, wakati wa hafla ya kuwatunuku vyeti na zawadi mbalimnbali wanafunzi waliofanya vizuri kitaaluma kuelekea mahafali yanayotarajiwa kufanyika leo Ijumaa.
Kwenye hafla hiyo wanafunzi wa chuo hicho walionyesha vipaji mbalimbali kwa kubuni vitu mbalimbali kwenye maeneo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano TEHAMA.
Prof Lwoga alisema chuo kitafanya kila linalowezekana kuhakikisha vipaji hivyo vinaendelezwa lakini aliwasihi
wahitimu kuamini katika kile wanachofanya ili kuweza kutengeneza fursa za ajira mara wanapohitimu.
“Tunafurahi kusherekea mafanikio na maendeleo ya kutimiza miaka 60 na tangu chuo kimeanzishwa kimefanikiwa kuzalisha wataalamu wa biashara na wajasiriamali pamoja na kufanikiwa kuongeza mitaala 63 kwenye ngazi za Biashara,TEHAMA na Metrologia,” alisema.
Profesa Lwoga aliwashauri wahitimu kuendelee kujenga uwezo wa kujiajiri na kutumia teknolojia na ujuzi waliopata chuoni hapo kujiajiri na kuajiri wenzao badala ya kuhangaika kutafuta ajira kwenye kampuni mbalimbali wanapohitimu.
Naye Rais wa Sauti ya Wanawake Wajasiriamali, Maida Waziri, aliwataka wahitimu na wanafunzi walio wabunifu kusimamia ndoto zao licha ya kuwa na vikwazo katika safari ya mafanikio kwa kutoa muda na akili kwa kila wanachokifanya.
Alikiomba chuo hicho kuweka mpango wa kuwatambua na kuwaendeleza wahitimu wake waliobuni vitu mbalimbali kama alivyoona kwenye hafla hiyo kuhakikisha wanafika mbali.
“Nimetembelea maonyesho mbalimbali nimeona namna wanafunzi wenu walivyo wabunifu wa bidhaa mbalimbali kwa hiyo ninachoomba ni kwamba hakikisheni hawa wanatimiza ndoto zao, hivi vitu wanavyobuni viendelezwe,” alisema
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED