BoT yapigilia msumari onyo matumizi ya fedha za kigeni

By Halfani Chusi , Nipashe
Published at 11:08 AM Jan 09 2025
news
Picha: Mtandao
Dola za Marekani.

BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imewaonya wanaotumia fedha za kigeni kufanya miamala nchini ikisisitiza kufanya hivyo ni kuhujumu uchumi wa nchi na ni kosa kisheria.

Pia imesema Kikao cha Kamati ya Sera ya Fedha kimeamua kuendelea na kiwango cha Riba ya Benki Kuu (CBR) cha asilimia sita katika robo ya kwanza ya mwaka 2025.

Gavana wa BoT, Emmanuel Tutuba, alisema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati akitoa taarifa  ya kamati sera ya fedha kuhusu riba ya Benki Kuu kwa kipindi cha robo ya kwanza kwa mwaka 2025.

Alisema mtu anapofanya miamala ya ndani ya nchi, anatakiwa kutumia saratu ya Tanzania  na kusisitiza kuwa  anayefanya kinyume, anahujumu uchumi wa nchi kwa sababu anatumia sarafu za nchi zingine.

Kuhusu kutokubadili riba, alisema, uamuzi huo unalenga kuhakikisha kiwango cha ukwasi kinaendelea kuwa cha kutosha katika uchumi, kudhibiti mfumuko wa bei kubaki chini ya lengo la asilimia tano na kuwezesha kuongezeka kwa kasi ya ukuaji wa uchumi kufikia takriban asilimia 5.7 katika robo ya kwanza ya mwaka 2025.

Aliongeza uamuzi huo unalenga kuwa na utulivu wa thamani ya shilingi dhidi ya fedha za kigeni ili kuendelea kuwa na mfumuko wa bei ndogo utakaochangia jitihada za kuwafanya wananchi kutofanya miamala yao kwa kutumia fedha za kigeni nchini.

Kuhusu mwenendo wa uchumi wa dunia, alisema kamati ilibaini kuwa ripoti zilizotolewa na Shirika la Fedha Duniani (IMF) na Benki ya Dunia, zinaonesha ukuaji wa uchumi unakadiriwa kuwa imara katika mwaka 2024.

Alisema katika robo ya nne ya mwaka 2024, kamati ilibaini mazingira ya uchumi duniani yaliimarika kwa kiwango kikubwa, kasi ya ukuaji wa uchumi iliongezeka, mfumuko wa bei uliendelea kupungua katika nchi nyingi, na mazingira ya upatikanaji wa fedha kwa riba nafuu katika masoko yaliimarika.

Mazingira mazuri ya kiuchumi, alisema yanatarajiwa kuendelea katika robo ya kwanza ya mwaka 2025 kutokana na ongezeko la mahitaji ya walaji, sera wezeshi za bajeti na kuimarika kwa mazingira ya upatikanaji fedha kwa riba nafuu huku akihadharisha kwamba yanaweza kuathiriwa na migogoro ya kisiasa duniani na mivutano ya kibiashara kuongezeka.

“Uchumi wa Tanzania Bara na Zanzibar umeendelea kuwa imara kwa mwaka 2024. Uchumi wa Tanzania Bara ulikua kwa asilimia 5.4 katika nusu ya kwanza ya mwaka 2024 na unatarajiwa kukua kwa asilimia 5.6 katika robo ya tatu na asilimia 5.7 katika robo ya nne ya mwaka 2024.

“Kwa kuzingatia mwenendo huo, ukuaji wa uchumi unatarajiwa kuwa sawia na matokeo ya ukuaji wa asilimia 5.4 kwa mwaka 2024. Ukuaji huu umechangiwa zaidi na ongezeko la shughuli za kilimo, usafirishaji, ujenzi, na biashara,” alisema Tutuba.

Kwa upande wa Zanzibar, alisema uchumi ulikua kwa asilimia 6.8 katika robo ya kwanza na asilimia 7.2 katika robo ya pili ya mwaka 2024 na ulikadiriwa kukua kwa viwango hivyo kwa robo mbili zinazofuata, hivyo kufikia matokeo ya ukuaji wa asilimia 7.2 kwa mwaka 2024.

Alizitaja shughuli zilizochangia kukua kwake kuwa ni pamoja na utalii, ujenzi, na viwanda na kwamba katika mwaka huu, ukuaji wa uchumi kwa Tanzania Bara na Zanzibar unatarajiwa kuendelea kuwa wa kasi ya kuridhisha, kwa takriban asilimia sita na asilimia 6.8, mtawalia.

“Ukuaji huu unatarajiwa kuchangiwa na ongezeko la uzalishaji katika shughuli za kilimo, utekelezaji wa miradi ya ujenzi, maboresho katika usafirishaji na ugavi, nishati ya uhakika, pamoja na utekelezaji wa sera za fedha na kibajeti.

“Ukuaji wa fedha na mikopo kwa sekta binafsi uliendelea kuwa wa kasi ya kuridhisha mwaka 2024, ambapo ulifikia wastani wa asilimia 12.5 na asilimia 16.9, mtawalia,” alifafanua Tutuba.

Alisema ukwasi wa fedha za kigeni uliongezeka kwa kiwango kikubwa katika robo ya nne ya mwaka 2024.  Hali iliyotokana  na kuimarika kwa mazingira ya upatikanaji fedha duniani kutokana na kupungua kwa riba katika nchi zinazoendelea na kuongezeka kwa mapato ya fedha za kigeni nchini kutokana na shughuli za utalii, mauzo ya dhahabu, korosho na tumbaku.

Pia alisema thamani ya shilingi inatarajiwa kuwa imara katika robo ya kwanza ya mwaka 2025, kutokana na kuwapo kwa ukwasi wa kutosha wa fedha za kigeni uliopatikana katika robo ya nne ya mwaka 2024, utekelezaji wa sera ya fedha kutokana na uamuzi wa kubakiza Riba ya Benki Kuu kuwa asilimia sita na bei za bidhaa katika soko la dunia kuwa nafuu.