NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko amesema serikali imetenga Sh.bilioni 118 kwa ajili ya kupeleka umeme kwenye maeneo ya wachimbaji wadogo nchini.
Amesema katika fedha hizo, Mkoa wa Geita umetengewa Sh. bilioni saba.
Dk. Biteko alitoa kauli hiyo juzi mkoani Geita wakati akizindua Maonesho ya Saba ya Kitaifa ya Teknolojia ya Madini yaliyofanyika katika viwanja vya EPZA Bomba Mbili.
Alisema hatua hiyo itasaidia kuondoa adha ya wachimbaji wadogo kutumia gharama kubwa kuendesha mitambo na shughuli zao zinazohitaji umeme kwa kutumia majenereta.
Aidha, aliwataka wachimbaji na wafanyabiashara wa madini kushirikiana vyema na serikali kwa kuuizuia Benki Kuu ya Tanzania (BoT) asilimia 20 ya madini kabla ya kuyauza na kuyasafirisha kwenda nje.
Katika hatua nyingine, Dk.Biteko aliridhishwa na huduma zinazotolewa na Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), kwa kuwafikia wafanyabiashara na wachimbaji kwa kutoa huduma na hamasa ya kurasimisha biashara zao.
Naye, Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, alisema katika kuboresha sekta ya madini serikali imeongeza bajeti yake kutoka Sh. bilioni 90 hadi kufikia Sh.bilioni 231 kwa mwaka 2024|25 ambapo bajeti hiyo imeelekezwa katika ununuzi wa helkopta, ujenzi wa maabara mbili ambayo moja itajengwa mkoani Geita.
Aidha, alipiga marufuku raia wa kigeni kuwekeza uchimbaji katika migodi yenye leseni ya uchimbaji mdogo na kuwa hali hiyo imekuwa ikisababisha migogoro ya mara kwa mara.
Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martine Shigela alisema kwa kipindi cha miaka mitatu leseni 316 zimetolewa kwa wachimbaji mkoani humo.
Alisema kuwa kati ya leseni hizo 30 zimetolewa kwa wanawake, huku wachimbaji wadogo wakizalisha zaidi kilo 16,000 za madini na kulipa kodi ya serikali zaidi ya Sh.bilioni 165.
Alisema maadhimisho hayo kwa mwaka jana yalikuwa na washiriki 350 kutoka mikoa mbalimbali na wengine kutoka nje ya Tanzania na kuwa mwaka huu wameshiriki zaidi ya 800.
Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji wa Madini nchini (FEMATA), John Bina, alisema wamekubaliana wachimbaji na wanunuzi kuiuzia BoT asilimia 20 ya madini wanayopata kabla ya kuuza na kuyasafirisha.
Ofisa Leseni Mwandamizi kutoka BRELA, Koyan Aboubakar alisema dira ya wakala huo kwa sasa ni kuwafikia wadau wengi zaidi pamoja na kutoa huduma za papo kwa papo.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED