ATCL yarejesha safari za Iringa, kuanza Februari 22

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 12:01 PM Feb 14 2025
Ndege ya Tanzania.
Picha: Mtandao
Ndege ya Tanzania.

KAMPUNI ya Ndege Tanzania (ATCL) imerejesha safari za moja kwa moja kati ya Dar es Salaam na Iringa, baada ya kukamilika kwa ukarabati wa Uwanja wa Ndege wa Iringa.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano kwa Umma kutoka ATCL, safari zitaanza Jumamosi (Februari 22), saa 3:00 asubuhi katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere na kutua katika Uwanja wa Ndege wa Iringa ndani ya dakika 60, kwa kutumia ndege aina ya DHC Q400, yenye uwezo wa kubeba abiria sita daraja la biashara na 70 daraja la kawaida.

Taarifa hiyo ilisema nauli ya safari ya kwenda na kurudi kati ya Dar es Salaam na Iringa itakuwa Sh. 199,200 ambayo inajumuisha usafirishaji wa mzigo wenye uzito wa hadi kilo 23 kwa sehemu ya mizigo, pamoja na begi la mkononi lisilozidi kilo saba, bila malipo ya ziada. 

“ATCL itaanza na safari tatu kwa wiki, kila Jumatatu, Jumatano na Ijumaa ambapo wanachama wa Twiga (Twiga Members) wataweza kulipia tiketi kwa kutumia pointi zao za safari,” ilisema taarifa hiyo. 

Aidha, kwa watakaojisajili kwenye Mpango wa Wasafiri wa Mara kwa Mara kupitia Aplikesheni ya Simu ya Air Tanzania (Air Tanzania Mobile App), watazawadiwa papohapo pointi 3,000 ambazo wataweza kuzitumia kupata punguzo la nauli ikiwa watakata tiketi zao kupitia ATCL. 

Ilitaja njia za kukata tiketi ni pamoja na tovuti: www.airtanzania.co.tz, Aplikesheni ya simu ya Air Tanzania, Kituo cha Huduma kwa Wateja ambacho kinatoa huduma kwa saa 24 kila siku (+255748773900) au kutembelea Ofisi za ATCL zilizopo ndani na nje ya nchi.

“Kurejeshwa kwa safari hizi kutaboresha muunganiko wa usafiri kwa wafanyabiashara, watalii, wakazi wa Mkoa wa Iringa na wasafirishaji wa mizigo na mazao kutoka Iringa na mikoa jirani, hivyo kufungua fursa mpya za kibiashara,” ilisema taarifa hiyo.