SERIKALI ya Zanzibar imesema utekelezaji wa Mkataba wa Eneo Huru la Biashara Afrika (AfCFTA), katika kuondoa vikwazo visivyokuwa vya kiushuru na kufungamanisha sera za biashara kutasaidia kupatikana kwa soko la bidhaa za Tanzania nje ya nchi.
Hayo yalisemwa jana na Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara, Dk. Hashil Abdallah, wakati wa ufunguzi wa mkutano wa 17 makatibu wakuu wa AfCFTA unaofanyika visiwani Zanzibar.
Mkutano huo unafuatiwa na mkutano ngazi ya mawaziri utakaofanyika Juni 24 – 25, visiwani Zanzibar, ambapo Tanzania ni mwenyekiti wa mikutano ya ngazi zote kwa mwaka 2024.
Aidha, Dk. Abdallah alisema kuwa bainisha kuwa utekelezaji wa AfCFTA nchini kutachangia kuhamasisha ukuaji wa viwanda na kuboresha mazingira ya biashara, ambako kutatoa matokeo chanya kwa kuongeza ajira na kuongeza pato la taifa.
Alisema kutachangia pia kutoa huduma bora za kijamii kwa Watanzania na hatimaye kufikia malengo ya Dira ya Taifa 2025 na Agenda 2063 ya Afrika yenye maendeleo.
Vilevile, alitoa wito kwa Jumuiya za Wafanyabiashara wa Tanzania kuchangamkia fursa za soko la AfCFTA lenye watu zaidi ya Sh.billioni 1.3 kwa kuzalisha bidhaa zenye ubora na viwango vinavyotakiwa zinazoweza kushindana katika soko hilo.
Alisema wakifanikiwa kufanya hivyo watakuwa wanatekeleza kwa vitendo dhamira ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kufungua nchi kiuchumi, kibiashara na kiuwekezaji.
“Wenzetu wanakimbia sisi tunatakiwa kukimbia zaidi na ni jukumu letu sasa watanzania kuchangamkia fursa zilizopo katika mkataba wa AfCFTA na hapo ndipo tutakuwa tunatekeleza kwa vitendo, ile dhamira ya Rais Samia katika jitihada zake katika kufungua nchi kiuchumi, kibiashara na kiuwekezaji,”alisema Dk. Abdallah.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda Zanzibar, Fatma Mabrouk Khamis, aliwataka makatibu wakuu hao wa biashara kuhakikisha wanatimiza malengo ya AfCFTA katika kuunda Afrika yenye ustawi na jumuishi, ili kuhakikisha wananchi wa kila nchi wananufaika na manufaa ya AfCFTA yanagawanywa kwa usawa bila kuacha nchi mwananchama yoyote nyuma.
Aidha, alitoa wito kwa wananchi wote hususani wananwake na vijana wa Tanzania Bara na Visiwani kuchangamkia fursa hizo kwa kuuza bidhaa zenye ubora na zenye asili ya Tanzania kulingana na mahitaji ya soko hilo linalojumisha nchi 54 za Afrika.
Alisema wakichangamkia soko hilo wataongeza ajira kwa kuwa AfCFTA inatoa fursa ya kuuza bidhaa au huduma ndani ya Bara la Afrika, bila vikwazo vyovyote vya kiushuru kwa nchi yoyote Afrika ambayo ni mwanachama.
Akitoa mfano wa bidhaa za mwani zinazotengenezwa kwa wingi Zanzibar, Fatma alisema kutokana na fursa za AfCFTA, bidhaa hizo zinauzwa Uganda, Congo na nchi nyingine za Afrika.
Alisema kampuni zinazosafirisha bidhaa hizo zimepatiwa mafunzo ya kuelewa mahitaji ya soko na kuhakikisha bidhaa zao zinafikia viwango vinavyohitajika.
“Mkataba huu wa AfCFTA unatulazimisha nchi za Afrika kuboresha mazingira ya biashara, kuondoa vikwazo visivyo vya kiushuru, kujenga miundombinu na kuboresha sheria zetu ili kupanua wigo wa soko, kuvutia wafanyabiashara na wawekezaji katika sekta mbalimbali kama vile viwanda, kilimo, mifugo na ufugaji, hali ambayo inaongeza ajira, Pato la Taifa na kukuza uchumi wa wananchi wetu na wa Taifa kwa ujumla,” alisema Fatma.
Mkurugenzi wa Huduma za Biashara,Uwekezaji, Haki Mliki Bunifu na Biashara mtandao wa AfCFTA, Emily Ndoria, alisema AfCFTA imetengeneza Itifaki mbalimbali ambazo zinalenga kurahisisha utekelezaji wa AfCFTA na ufanyaji biashara kwa ujumla.
Alisema itifaki hizo zinaziwezesha nchi za Afrika kuuziana bidhaa na huduma baina ya nchi na nchi, kuongeza ajira, pato la taifa na kujitegemea kibiashara na kiuchumi.
Aidha, alizishauri nchi wananchama kuhamasisha wananchi wao hususani wanawake na vijana kutumia fursa zinazopatikana katika mkataba wa AfCFTA kwa kuzalisha bidhaa zenye ubora na viwango vya kimataifa ili ziweze kukidhi mahitaji na kushindana katika soko hilo muhimu la Afrika.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED