IMEZOELEKA miji na majiji makubwa kama Dar-es Salaam ni maeneo ya kutafuta maisha hivyo watu walio wengi wanatoka vijijini kupata maisha bora.
Wapo baadhi wanaingia mijini bila kuwa na ndugu wala mipango au fedha mfukoni za kuanza maisha mapya mjini.
Hivyo, wanalazimika kuingia mtaani na kufanya shughuli zao lakini wanalala nje kama vile chini ya madaraja mfano Ubungo, Kimara, TAZARA kwa Dar es Salaam.
Wapo wanaojisitiri kando ya barabara, nje ya vibanda vya biashara na maduka, pembezoni mwa nyumba za watu na kwenye masoko.
Wasaka maisha hawa wengine wanatuhumiwa kuwa wahalifu kuhusishwa na kuwaibia watu na wakati mwingine wanajeruhi na kupora.
Moja ya wajumbe wa serikali za mitaa kutoka Kisutu Dar-es Salaam, anaeleza kuwa mwaka 2024 watu wanaolala nje ni chanzo cha wizi kwani hawana cha kufanya.
Japo siyo wote ni baadhi lakini kutoka vijijini wanakuja mijini bila msaada, kazi wala fedha kunaweza kuwafundisha uhalifu.
Licha ya kwamba wizi ni tabia ya mtu binafsi anayoweza kutoka nayo kwao umaskini na kukosa chakula kunawapa mawazo na maamuzi ya kufanya chochote ili kupata riziki na chakula.
Uhalifu wanaojihusisha nao ni pamoja na kuvuta bangi, kutumia mihadarati na kupora mali za watu kama simu, pochi na hata pikipiki.
Pamoja na uhalifu pia ni chanzo cha uchafu mijini kwani hawana mahali rasmi pa kulala, kujisaidia na kupata huduma kama maji ya kuoga, kufua nguo na hivyo kujihudumia popote.
Wanaweza kufua mtoni, kupasua mabomba kupata maji, kwenda kwenye gereji hivyo kuchangia kuongeza taka na mazingira machafu mijini kwa kuwa hata wakila hutupa mabaki na vifungashio popote.
Kukosa huduma hizo kunachangia kujisaidia haja ndogo kwenye kuta za uzio, kutumia mifuko kujisaidia na kusababisha vinyesi kuzagaa huku baadhi wakitumia chupa za maji kwa ajili ya haja ndogo.
Tanzania ni nchi inayolenga kufikia kiwango cha juu cha maendeleo kiuchumi, hivyo inawajibika kuchukua hatua kukabiliana na hali duni ya vijana.
Kama lengo la Dira ya Maendeleo ya 2050 ni kuwa na maisha bora kwa kila Mtanzania isiwapuuze vijana kama hao na mchango wao.
Ikumbukwe kama nchi inawasahau vijana inaweza kujiweka katika hatari kubwa ya kukwama kimaendeleo, kutishia usalama na maadili kwa sababu ya kuwa na kundi kubwa la wahalifu ambao ni vijana wenye umri mdogo.
Katika dunia ya sasa na hata ndani ya siku zijazo za dira ya maendeleo ya 2050 kama nchi haitawekeza katika miradi ya kuinua maisha ya vijana hawatakuwa na nafasi ya kushindana na mataifa mengine katika sekta mbalimbali ili kufikia maendeleo endelevu.
Tanzania ina nafasi ya kujiandaa na kuimarisha maisha ya vijana kuanzia kiuchumi ikiwa itawekeza kikamilifu mikakati kwa kurejea sensa ya watu na makazi ambayo inasema vijana ni karibu nusu ya raia wa nchi hii.
Serikali ikumbuke vijana hawa ndiyo nguzo ya maendeleo ya nchi hii na lazima ifanye juu chini kuweka mikakati, mipango na sera madhubuti za kuboresha maisha yao, kwani ikitetereka na kuwaacha wajirundike mijini itakuwa imeweka msingi mbaya na kukwamisha dira ya maendeleo ya 2050.
Cha msingi ni kuwapatia elimu inayoendana na mabadiliko ya dunia ya kidijitali, kielektroniki na inayojaa ubunifu. Serikali ifanye hivyo kupitia mfumo mpya wa masomo wa kufundisha elimu ya amali, uanagenzi na kuhitaji kuwekeza zaidi katika teknolojia ili kufanikisha mitaala inayobadili maisha ya vijana.
Bila teknolojia, ubora wa elimu ambayo inapaswa kuwaandaa vijana kwa ujenzi wa taifa lao itakuwa vigumu kufanikisha dira 2050.
Lakini serikali ikumbuke kuwa kuwaelimisha watoto, vijana na Watanzania bila kuwapatia kazi ni kuongeza matatizo katika nchi ni lazima kujenga viwanda vidogo na vikubwa vijijini kutoa ajira.
Vijana wakikosa nafasi za kazi wanaweza kutumia elimu yao kuwa wahalifu na hii ni hatari kwa usalama wa nchi, wanaweza kuwa wezi, waharibifu wa mali na hata kutumia teknolojia kuyumbisha maendeleo ya taifa.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED