STRAIKA Prince Dube, raia wa Zimbabwe, ameweka rekodi ya kufunga mabao matatu maarufu 'hat-trick' na kuiongoza Yanga kupata ushindi wa mabao 3-2 katika mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Mashujaa FC iliyochezwa kwenye Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam jana.
Mbali na kuwa ni 'hat-trick'ya kwanza msimu huu, lakini pia Dube ndio alikuwa anafungua akaunti yake ya mabao kwa sababu hakuwahi kupachika bao lolote kabla ya mechi hiyo.
Staika huyo ambaye tangu ajiunge na Yanga mwanzoni mwa msimu alikuwa na ukame wa mabao kiasi cha kuzua mijadala mbalimbali katika mitandao ya kijamii na vijiweni kwa mashabiki wa soka, alichaguliwa pia kuwa mchezaji bora katika mchezo huo.
Bao la kwanza katika mechi hiyo alilifunga dakika ya saba, akiunganisha krosi ya upendo iliyopigwa na kiungo mshambuliaji, Pacome Zouzoua, ilikuwa ni kazi iliyoanzia kwa Aziz Ki aliyenyang'anya mpira kutoka kwa wachezaji wa Mashujaa, akakimbia nao umbali mrefu kabla ya kuupiga kwenye wingi ya kulia kwa Pacome, ambaye aliurudisha ndani na kumkuta mfungaji.
Dakika ya 21, Dube alipachika bao la pili kwa kichwa, akimalizia kazi kubwa iliyofanywa na Pacome, kufuatia uzembe uliofanywa na mabeki wa Mashujaa.
Mpira huo ulileta kizaazaa langoni, awali Clement Mzize alikuwa afunge lakini ukambabatiza mchezaji wa timu pinzani, kabla ya kumkuta Dube aliyeusukumizia wavuni kwa kichwa.
Alitimiza 'hat-trick' yake dakika ya 52, akiunganisha kwa mara nyingine mpira kwa kichwa, krosi kutoka kwa Kibwana Shomari.
Hata hivyo haukuwa ushindi rahisi kwa Yanga, kwa sababu ililazimika kupambana kuhakikisha inaulinda kwa juhudi zote huku Mashujaa ikifanikiwa kupata bao dakika moja kabla ya mapumziko.
David Ulomi, alifunga bao hilo la kwanza la Mashujaa kwa shuti la mbali la kushtukiza, licha ya juhudi za kipa wa Yanga, Khomeini Aboubakar, kuruka kutaka kuokoa, lakini mpira ulimshinda na kujaa wavuni.
Wakati Yanga ikiongoza kwa mabao 3-1, dakika 10 baada ya kupata bao la tatu, Idriss Stambuli, aliipatia Mashujaa bao la pili ambalo lilifanana sana kama la kwanza kwa wageni hao.
Akiwa umbali wa mita takriban 35 hivi, aliachia shuti kali ambalo Khomeini alitaka kulidaka, lakini lilimshinda nguvu na kutinga wavuni.
Ushindi huo unaifanya Yanga kupanda hadi nafasi ya tatu katika msimamo wa ligi hiyo ikifikisha pointi 30 sawa na Singida Black Stars, ikibebwa na uwiano mzuri wa mabao ya kufunga na kufungwa.
Mechi ilianza kwa kasi, ambapo dakika ya pili tu ya mchezo Yanga walikosa bao la wazi, wachezaji wake wawili, Stephane Aziz Ki, na Mzize walikosa bao, kila mmoja akitaka kuupachika wavuni bila mafanikio.
Krosi iliyopigwa na Yao Kouassi ilimkuta Aziz Ki ambaye aliunganisha shuti dhaifu lililowababatiza mabeki wa Mashujaa, ukamrudia Mzize ambaye alipiga mpira nje.
Dakika tatu baadaye, Duke Abuya nusura aipatie Yanga bao, kwani baada ya kupata pasi kutoka kwa Aziz Ki, alipiga shuti kali la mbali, lakini lilipaa juu.
Abdulnasir Mohamed Gamal, aliikosesha Mashujaa bao la wazi alipobaki yeye na Khomeini, lakini alichelewa kufanya maamuzi na kukutwa na mabeki wa Yanga akiwa bado hajaupiga mpira, wakaokoa.
Ligi hiyo inatarajiwa kuendelea tena kesho kwa Kagera Sugar kuikaribisha Simba kwenye Uwanja wa Kaitaba ulioko Bukoba mkoani, Kagera.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED