Simba, Mashujaa vitani

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 08:15 AM Nov 01 2024
Wachezaji wa Simba wakishuka kwenye ndege baada ya kuwasili mkoani Kigoma.
Picha: Mtandao
Wachezaji wa Simba wakishuka kwenye ndege baada ya kuwasili mkoani Kigoma.

TAHADHARI na umakini ndio mambo muhimu yaliyoko katika akili ya Wekundu wa Msimbazi ambao wanatarajia kukutana na wenyeji Mashujaa FC katika mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara itakayochezwa leo kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika mkoani, Kigoma.

Simba inahitaji kupata ushindi wowote ili kupanda hadi nafasi ya pili katika msimamo wa ligi hiyo kutokana na kuwa na mabao mengi ya kufunga.

Simba imefunga mabao 16, ikifungwa matatu, huku Singida Black Stars ikiwa na mabao 13, zote zikiwa zimeruhusu nyavu zao kutikiswa mara tatu.

Akizungumza na gazeti hili jana, Kocha Mkuu wa Simba, Fadlu Davids, amesema kikosi chake kipo tayari kwa ajili ya mchezo huo na malengo yao ni kupata pointi tatu ili kujiimarisha katika msimamo wa ligi hiyo.

Fadlu alisema anatarajia mechi hiyo itakuwa ngumu lakini wachezaji wake wamejipanga kuonyesha kiwango cha juu baada ya kupata mapumziko tofauti na walivyokuwa katika michezo iliyotangulia.

Simba ilipata mapumziko ya wachezaji wake baada ya kutocheza mchezo uliotakiwa kufanyika Jumanne iliyopita kwenye Uwanja wa KMC, Dar es Salaam dhidi ya JKT Tanzania, ambayo walipata ajali.

"Mchezo utakuwa mzuri, utakuwa mgumu kwa sababu Mashujaa ni timu nzuri, hata msimamo wa ligi unaonyesha hivyo, inashika nafasi ya sita, ile tumejipanga vizuri, wachezaji wangu wamepumzika vya kutosha, nadhani wengi watarudi katika viwango vyao halisi," alisema kocha huyo.

Hata hivyo alisema katika mchezo wa leo bado atawakosa wachezaji wake wawili, ambao ni beki wa kati, Abdulrazack Hamza na Yusuph Kagoma, walioumia katika mchezo dhidi ya Yanga.

"Afadhali Hamza, anaweza kurejea mapema, ila Kagoma anaweza asionekane hata katika mchezo unaofuata dhidi ya KMC, " Fadlu alisema.

Naye Kocha Msaidizi wa Mashujaa, Maulid Makata, alikiri mchezo utakuwa mgumu kwa sababu wanakutana na timu kubwa lakini msimu huu ikiwa bora zaidi kuliko msimu uliopita.

Makata alisema hata hivyo wachezaji wake wanapenda kucheza mechi za aina hiyo ambazo zinawatazamaji wengi uwanjani na katika televisheni.

"Mechi kama hizi makocha kazi yetu ni kuwajenga tu kisaikolojia kwa sababu wachezaji wenyewe wanazitaka, wanajua zinaonekana na watu wengi kwa hiyo nao wanataka waonekane, wajiuze.

Tunajua wenzetu ni timu kubwa na wana maandalizi makubwa kuliko sisi, huwezi kutulinganisha na sisi, ukiangalia malengo yao ni kutwaa ubingwa na sisi kubaki Ligi Kuu au nafasi ya nne, ila katika mpira chochote kinaweza kutokea," aliongeza  kocha huyo.