TFS kutumia ndege nyuki kudhibiti uharibifu wa misitu

By Hamida Kamchalla , Nipashe
Published at 01:40 PM Dec 20 2024
Ndege nyuki.

WAKALA wa Misitu Tanzania (TFS) Kanda ya Kaskazini imeanza kutumia teknolojia ya ndege zisizo na rubani (drones) kubaini misitu iliyoharibiwa na shughuli za kibinadamu, hatua ambayo inalenga kudhibiti uharibifu wa rasilimali hizo kwa mujibu wa sheria.

Shughuli za kibinadamu, kama vile kilimo cha kuhama hama, uchomaji wa mkaa, na uchimbaji wa madini, zinatajwa kuwa changamoto kubwa inayohatarisha ustawi wa rasilimali za misitu katika maeneo mbalimbali nchini. Kutokana na hilo, TFS imetilia mkazo umuhimu wa kutumia drones kufuatilia na kutambua maeneo yaliyoharibiwa ili kuchukua hatua stahiki za kuwaondoa wavamizi na kurejesha hali ya asili ya misitu.

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga katika kikao cha wadau wa misitu, Mkuu wa Wilaya ya Korogwe, Willium Mwakilema, amesisitiza kuwa serikali ya mkoa itahakikisha wavamizi wote waliopo ndani ya misitu wanaondolewa mara moja.

“Shughuli za kibinadamu kwenye hifadhi za misitu ni tishio kubwa. Tunatambua kuwa kilimo cha kuhama hama, uchomaji wa mkaa, na uchimbaji wa madini ni sehemu ya changamoto hizi, lakini hatutaacha kuhakikisha kuwa misitu yetu inalindwa kwa gharama yoyote,” amesema Mwakilema.

Kwa hatua hiyo ya kiteknolojia, TFS inatarajia kuboresha usimamizi wa rasilimali za misitu kwa kufanikisha ufuatiliaji wa maeneo makubwa kwa ufanisi zaidi na kuhakikisha kuwa hatua za kisheria zinachukuliwa dhidi ya wale wote wanaokiuka sheria za uhifadhi wa mazingira.