Mzize atabiri bao lake bora Afrika

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 09:30 AM Jan 07 2025
 Clement Mzize (kulia)
Picha: Mtandao
Clement Mzize (kulia)

STRAIKA wa Yanga, Clement Mzize, amefunguka kuwa hajawahi kufunga bao bora na zuri katika historia yake ya soka kama alilolifunga katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, uliochezewa Jumamosi iliyopita, Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Mzize, ambaye alipachika mabao mawili katika mchezo huo hatua ya makundi, moja likiwekwa wavuni na Stephane Aziz Ki, alisema bao la kusawazisha alilolifunga dakika ya 33, linaingia kwenye kumbukumbu ya bao namba moja kwa ubora kati ya yote aliyoyafunga, huku akitabiri kuwa huenda likaingia kwenye kinyang'anyiro cha bao bora na kushinda.

Straika huyo ambaye anaichezea pia Timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, aliupata mpira karibu na katikati ya uwanja, upande wa Mashariki ya Uwanja, akaanza kuukokota bila kubugudhiwa na mchezaji yeyote, alivyoona hivyo aliamua kuachia shuti kali la mbali, umbali wa takriban yadi 35 na kwenda kujaa juu ya maungio ya mwamba wa juu na nguzo ya chini, huku kipa, Alioune Badara Fatty, akiruka bila mafanikio.

Lilikuwa ni bao la kusawazisha baada ya kufungwa la kwanza na kipa Badara, dakika ya 16 kwa mkwaju wa penalti.

"Sijawahi kufunga bao kama lile, ni mara ya kwanza tangu nianze soka, hata huko mchangani ambako sijawahi kuonekana sikufunga bao la namna ile hata mara moja.

"Nimewahi kufunga mabao, lakini si kama lile, ni bao ambalo limeingia kwenye historia yangu, awali niliona la kawaida tu, mechi ilivyoisha kila mtu nasikia analizungumzia, ikabidi na mimi niende kuliangalia upya, ni bao zuri, huwezi kujua, linaweza kuingia katika orodha ya mabao bora Ligi ya Mabingwa Afrika au likashinda kabisa, tuombe Mungu, inawezekana likawa bao bora Afrika," alisema Mzize.

Kuhusu bao la pili alisema halikuwa na maajabu sana kwa sababu ni vitu ambavyo huwa wanavifanyia kazi mazoezini.

"Bao la pili nililofunga ni vitu ambavyo tumekuwa tukivifanya mazoezini ni kama vinajirudia tu, yale tunafunga sana," alisema Mzize.

Wakati huo huo, Kocha Mkuu wa Yanga, Sead Ramovic, ameweka wazi mbinu aliyoifanya hadi kuifunga TP Mazembe na kuchupa hadi nafasi ya tatu ya msimamo wa Ligi ya Mabingwa Afrika Kundi A, ikifikisha pointi nne.

"Kwa sasa tunacheza kwa kasi, tunakimbia pamoja, hakuna beki, mshambuliaji wala kiungo, kila mmoja anapaswa kukimbia mbele au nyuma na kumnyima mpinzani nafasi kwenye wakati sahihi.

Tuna wiki nne sasa tumekuwa imara, wachezaji wangu wamekuwa na nidhamu na kujituma, hicho ndicho kilichoikuta TP Mazembe na isingeweza kukiepuka kipigo kwa namna yoyote, hata timu zingine pia nadhani hazitotuonea tena kama ilivyokuwa awali," alisema kocha huyo raia wa Ujerumani.

Wakati Yanga ina pointi nne, MC Alger ya Algeria, juzi ilitoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Al Hilal ya Sudan, matokeo ambayo yamewafanya Waalgeria hao kubaki nafasi ya pili kwa kufikisha pointi tano, Al Hilal ikiendelea kuongoza kwa pointi 10.