UKUAJI wa mtoto kibaiolojia huanza kuhesabiwa tangu siku ya kwanza mimba inapotungwa. Wataalamu wa afya wanazitaja siku 1,000 za ukuaji huo kuwa muhimu zaidi kwa afya ya mama na mtoto.
Wiki 36 na kuendelea kwa ujauzito zimo katika siku 1,000 zinazotajwa kuwa muhimu katika ukuaji wa mtoto tangu tumboni mwa mama hadi anapofikisha umri wa miaka miwili.
Inapotokea tofauti katika ukuaji huo, ikiwamo mama kuathiriwa na mazingira yanayomzunguka kiuchumi na kijamii, athari huwa kwa mama na mtoto moja kwa moja.
Magonjwa ya akili kama vile sonona, ni miongoni mwa changamoto ambazo baadhi ya wajawazito na mama aliyetoka kujifungua hukumbana nayo na kuathiri ukuaji wa mtoto kiafya.
Kama ilivyoelezwa na wasaikolojia tiba kutoka Hospitali ya Saifee, mkoani Dar es Salaam, elimu ya afya ya akili kwa mama kabla na baada ya kujifungua, hupunguza madhara yatokanayo na sonona.
Wataalamu hao wanasema athari za sonona kipindi cha ujauzito na baada ya mama kujifungua zisipotibiwa mapema, huathiri mtoto aliyeko tumboni na akishazaliwa husababisha mtoto kuwa na uhusiano duni kijamii.
Kwa mujibu wa wataalam hao, sonona kwa mjamzito huvunja muunganiko wa mapenzi kati ya mama na mtoto. Muunganiko wa kihisia na kimwili ambao huanza wakati wa ujauzito na kuendelea katika maisha ya mtoto, wanautaja ni muhimu ili jamii kuwa na kizazi kilicho na upendo, weledi na matokeo chanya.
Mabadiliko ya homoni kwa kipindi cha ujauzito, kama ilivyoelezwa na wataalamu hao kwa Nipashe, ni jambo la kawaida kwa mjamzito, ingawa yakichukua muda mrefu humwathiri yeye na kiumbe kilichomo tumboni.
Kuna angalizo lingine -- sonona huonekana kwa dalili tofauti kwa kipindi cha wiki mbili, kama vile mtu kukata tamaa, kukosa usingizi ama kulala kupitiliza, kushtuka usingizini, kula zaidi au kula kidogo. Wengi wa wanaougua, chanzo kikuu ni ugomvi kati ya mtu au jamii inayomzunguka kwa muda mrefu.
Lipo angalizo lingine linalotia simanzi kutoka kwa wataalam --duniani asilimia 60 ya wajawazito hupitia sonona. Faraja pekee iliyopo ni kwamba ugonjwa huo unatibika kwa elimu ya saikolojia tiba au dawa.
Nipashe tunaungana na wataalam hao kuitaka jamii kuchukua hatua kukabiliana na sonona kwa wajawazito, ikizingatiwa takwimu zinaonesha mmoja kati ya kinamama saba hukumbwa na tatizo hilo.
Huzuni kupitiliza, kukosa hamu ya kula, kupungua au kuongezeka uzito na hofu, hasa hofu pale muda wa kujifungua unapokaribia, vinatajwa na wataalam kuwa hatari zaidi kwa afya ya akili.
Kwa mujibu wa wataalam hao, mtoto akizaliwa na mama mwenye shida hiyo, atakosa muunganiko kwa jamii, atakosa uhusiano wa kijamii, atachelewa kukua na kusumbuliwa.
Hivyo, ni muhimu jamii ikumbatie malezi bora kwa mjamzito na baada ya kujifungua, vyote vikitajwa na wataalam huwa chachu ya afya kiakili kwa mama, mtoto na jamii kwa kuwa maandalizi ya ukuaji wa mtoto huanza tangu siku ya kwanza mimba ilipotungwa.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED