KUSITISHWA kwa mgogoro kati ya Israel na kundi la Kipalestina la Hamas, kwenye Ukanda wa Gaza, uliodumu kwa takribani mwaka mmoja na miezi mitatu, kunakuja siku moja baada ya Rais Donald Trump, kutinga Ikulu ya White House.
Mgogoro huo umeacha athari za kiuchumi, kijamii na kiafya kwa siku 467. Shirika la Afya Duniani (WHO), linasema takribani robo ya waliojeruhiwa, watu 22,500 majeraha ni makubwa.
Kila siku watoto 10 hupoteza mguu mmoja au yote miwili. Upasuaji na ukataji wa viungo uliohitajika, ulifanyika kwa kiwango kidogo au bila ganzi.
Mazingira pia yameathiriwa na kuhatarisha afya za viumbehai, tani 85,000 za vilipuzi zilitupwa kwenye ardhi kwa miezi 15 huko Gaza.
Shirika la Umoja wa Mataifa linalowahudumia Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA), linasema kila siku watoto 10 hupoteza mguu mmoja au yote miwili.
Hata hivyo, upasuaji na ukataji wa viungo hufanyika kwa kiasi kidogo au bila ganzi kabisa.
Inakadiriwa tani 85,000 za vilipuzi zimetupwa huko Gaza, kulingana na Mamlaka ya Ubora wa Mazingira ya Palestina.
Marekani ni mshirika muhimu wa Israel. Utekelezaji wa makubaliano ya kusitisha mgogoro huo, unakuja baada ya Israel na Hamas, kukubali kusitisha vita huko Gaza, kwa kukubaliana kuwaachilia huru mateka wa pande hizo mbili.Marekani na wapatanishi wengine akiwamo Qatar wanasema, ni kwa mujibu wa Aljazeera, yatakuwa mafanikio makubwa zaidi tangu miezi 15 ya vita, kupita.
Kundi la Wapalestina lenye silaha la Hamas liliishambulia Israel, Oktoba mwaka juzi.
Huku Trump akiingia mamlakani rasmi wiki hii, awali katika mkutano wa ushindi uliofanyika mwishoni mwa mwaka jana, mjini Washington, Marekani, alijipatia sifa kwa kuachiwa kwa mateka wa kwanza kutoka Gaza, akimpuuza mtangulizi wake Joe Biden, ambaye pia alichukua sifa kwa makubaliano hayo.
Kadhalika, Trump alitoa sifa kwa mjumbe wake mpya wa Mashariki ya Kati, Steve Witkoff.
MATEKA WAACHIWA
Mapema wiki hii, Israel iliwaachia huru wafungwa na mahabusi 90 wa Kipalestina. Lilikuwa ni tukio la saa chache baada ya mateka watatu wa Israel, kuachiliwa kutoka mikononi mwa Hamas huko Gaza na kurejea nchini mwao.
Kusitishwa mapigano kulianza kutekelezwa Jumapili iliyopita huku Waziri Mkuu wa Qatar, Sheikh Mohammed bin Abdul Rahman Al Thani, akisema makubaliano hayo kuanza kutekelezwa Jumapili yalipoiidhinishwa ni jambo jema.
Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, anasema kuna vifungu kadhaa ambavyo havijafafanuliwa, ambavyo alikuwa ana matumaini ya kukamilishwa leo jioni.
Mkataba uliokamilika utafanya vita huko Gaza kusitishwa na kubadilishana mateka na wafungwa. Hamas iliwakamata mateka 251 ilipoishambulia Israel Oktoba, 2023.
Inawashikilia mateka 94, ingawa Israel inaamini kuwa ni 60 pekee walioko hai. Kadhalika, Israel inatarajiwa kuwaachilia wafungwa 1,000 wa Kipalestina, baadhi yao wamefungwa kwa miaka mingi, ili kuwalipa mateka hao. Kwa mujibu wa BBC.
Ikiwa usitishwaji wa mapigano utaendelea, kubadilishana kwa mateka kunatarajiwa kufanyika tena Jumamosi hii Januari 25, inaongeza BBC.
Hamas inapaswa kuwaachilia mateka wanne wa kike waliokuwa hai. Kwa malipo, Israel itawaachilia huru wafungwa 30 hadi 50 wa Kipalestina, kwa kila mateka.
USHUHUDA WA MATEKA
Mmoja wa mateka aliyeachiwa huru, mwanafunzi wa udaktari Mpalestina, amejumuishwa miongoni mwa wafungwa 90 walioachiwa huru na Israel. Kituo cha habari cha Aljazeera kinataarifu.
Anasema hali ya kizuizini ilikuwa mbaya na kwamba upatikanaji mdogo wa chakula pamoja na maji umezidi.
Hata hivyo, Bara’a Al-Fuqha (22), anasema alihisi ahueni na furaha kubwa kuungana tena na familia yake, huko Ukingo wa Magharibi, Jumatatu hii.
Alipokutana na familia yake, aliwakumbatia, kuwashika kutoka kwenye basi la Chama cha Msalaba Mwekundu na kuingia katika umati wa Wapalestina walishangilia, wakiwakaribisha wafungwa kadhaa, wote wanawake na watoto, waliotoka gerezani.
CHANZO MGOGORO
Mamia ya wapiganaji wanaoongozwa na Hamas walifanya shambulizi ambalo halijawahi kushuhudiwa kusini mwa Israel, na kuvunja uzio wa mpaka na kulenga jamii, vituo vya polisi na kambi za jeshi.
Takribani watu 1,200 waliuawa na mateka zaidi ya 250 walirejeshwa Gaza. Hamas pia ilirusha maelfu ya makombora nchini Israel.
Israel ilijibu kwa kampeni kubwa ya kijeshi, kwanza kwa ndege na kisha uvamizi wa ardhini. Tangu wakati huo, Israel imeshambulia maeneo yote ya Gaza kwa njia ya ardhini, baharini na angani, huku Hamas ikiishambulia Israel kwa roketi.
Mashambulizi ya Israel yameiharibu Gaza na kusababisha uhaba mkubwa wa chakula, huku msaada ukijitahidi kuwafikia wale wanaohitaji zaidi.
WAATHIRIWA
Zaidi ya watu 46,700 wakiwamo watoto 18,000, wameuawa na mashabulizi ya Israel, kulingana na Wizara ya Afya ya Gaza inayodhibitiwa na Hamas.
Pia zaidi ya watu 110,265 wamejeruhiwa huko Gaza kutokana na mgogoro huo. Hii ni sawa na mtu mmoja kati ya 20.
WHO, inasema takribani robo ya waliojeruhiwa, watu 22,500, wana majeraha makubwa yaliyobadilisha maisha yao na yanahitaji ukarabati wa kiafya na hawapati.
Majeraha makali ya viungo ni aina kuu ya majeraha yanayohitaji ukarabati.
Wataalamu wanakadiria kuwa inaweza kuchukua zaidi ya muongo mmoja, kusafisha vifusi vilivyoachwa na mashambulizi hayo, ambavyo vina zaidi ya tani milioni 42, kwa mujibu wa Mpango wa Maendeleo wa Umoja wa Mataifa (UNDP).
Hatari iliyoko kwenye kazi ya kuondoa vifusi, ni kushughulikia mabomu ambayo hayajalipuka.
Karibu watu milioni 1.9 huko Gaza wamelazimika kuhama ndani ya eneo hilo, na karibu asilimia 80 wanaishi katika makazi ya muda yasiyo na mavazi ya kutosha au kinga dhidi ya baridi.
Mashirika ya Umoja wa Mataifa, yanakadiria nusu milioni wako katika maeneo yanayokumbwa na mafuriko.
Mamlaka za Gaza zimesema takriban mahema 110,000 kati ya 135,000 yanayotumika kama makazi katika Ukanda wa Gaza, yamechakaa na hayafai tena kutumika.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED