Mwanasiasa wa miraba minne, licha ya kufariki dunia, Z’bar ina mzizimo wa kifo chake *2025 uchaguzi mkuu wa kwanza bila Hamad Na Mwinyi Sadallah, ZANZIBAR JAPO imetimia miaka minne, Zanzibar inaendelea kuwa na mzizimo wa kifo cha mwanasiasa mkongwe na aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Maalim Seif Shariff Hamad.
Maalim Seif amefariki Februari 17, 2021 katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, jijini Dar es Salaam, dua na sala za Watanzania ni kumwomba Mungu amweke mahali pema peponi. Jina la Hamad katika uga na viunga vya siasa na uongozi wa Zanzibar, Tanzania na Afrika Mashariki na Kati, si geni masikioni mwa wengi, ndiyo maana litabaki kuwa alama kuu na nembo isiyofutika kwenye harakati za demokrasia za vyama vingi na siasa za ushindani.
Ni mwanasiasa jabali aliyewahi kutokea na kuishi katika visiwa vya Zanzibar huku akipendwa mno na wafuasi wake, akiaminiwa kulikovuka mipaka na kuwa kiongozi aliyekuwa akisikizwa, huku watu wakimtii kuliko.
Kinachobakia ni kwamba halitafutika jina hilo kutokana na umaarufu aliokuwa nao katika maisha yake, upendo alioujenga katika jamii yake lakini pia, kuaminika kwake katika anga za siasa na diplomasia, kitaifa, kikanda na kimataifa. Maalim Seif hakuwa mwanasiasa wa barabarani, alikuwa kingunge na mwamba usiotikiswa katika uwanja wa siasa, shujaa mwenye mwitikio, mvuto na kipaji cha aina yake anapolizungumzia jambo.
Kwa kifupi alikuwa kivutio ‘crowd puller’. Katika siku za uhai wake alijaliwa kuwa mvumilivu, mtu mwepesi wa kusamahe, mstaarabu, mpenda mazungumzo ya mapatano, muafaka, maridhiano kwa njia za majadiliano. Licha ya kuwa mwanadiplomasia nguli, pia ni mwanademokrasia bingwa ambaye alikuwa tayari kujinyima yeye au kupoteza lolote lenye maslahi binafsi, ilimradi kunusuru majanga hatarishi yasitokee katika jamii.
Pamoja na kupita miaka minne baada ya kuondoka duniani na kupumzishwa kijijini alipozaliwa huko Mtambwe Nyali Mkoa wa Kaskazini Pemba, Maalim Seif anabaki kuwa nguzo imara kwa chama chake na mustakabali mzima wa siasa za Zanzibar.
Anaendelea kubaki kuwa kitabu kinachosomwa siku zote na watu kuendelea kujifunza na kujielimisha. Hakuwa tu mwanasiasa na kiongozi, lakini alikuwa baba mwema katika jamii yake, mpenda umoja na amani, kiungo na kiunganishi katika jamii, aidha hakuwa mtu mwenye matata akiishi kwa kuwawekea wengine chuki na mifundo moyoni. Hakuamini katika maisha ya dharau, kebehi, majigambo na pia hakuweka kinyongo moyoni mwake.
Anakumbukwa kuwa aliishi kwa malengo mahususi na mtu aliyejali zaidi utaifa na uzalendo wa kweli kwa ajili ya kutetea Zanzibar wakati wowote. Akihutubia taifa kwa njia ya televisheni, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Hussein Ali Mwinyi, miaka minne, iliyopita ndiye aliyetangaza kifo cha Maalim Seif.
Mwanasiasa huyo alifariki dunia akiwa katika Taasisi ya Magonjwa ya Moyo ya Jakaya Kikwete katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) alikokuwa amelazwa kwa takribani wiki nzima.
NI KIONGOZI
Katika maisha yake amewahi kuwa Waziri Kiongozi wa Serikali ya Zanzibar jukumu alilolifanya kuanzia mwaka 1984 hadi 1988, chini ya Rais Ali Hassan Mwinyi, baadaye akashika tena wadhifa huo chini ya Rais Idris Abdul Wakil.
Kiongozi huyu amegombea mara kadhaa urais wa Zanzibar kupitia Chama cha CUF baadaye kwa ACT-Wazalendo akiwa anapata kura nyingi lakini hakubahatika kutangazwa kuwa ndiye mshindi wa urais. Mara mbili katika historia ya maisha yake amekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar chini ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) ambayo iliundwa zikiwamo juhudi zake za kuleta umoja Zanzibar.
Kama timu ya mpira Maalim Seif alikuwa na uwezo wa kucheza namba yoyote kwa umakini wake, wakati na muda alipohitajiwa kufanya hivyo.
Maalim Seif amefariki lakini bado yupo hai katika siasa za Tanzania kutokana na msingi ambao aliujenga katika maisha yake hakuwa mchoyo katika maarifa na kuwajenga wanasiasa chipukizi ambao sasa wameshika nafasi yake lakini si kwa kiwango chake.
Anaacha mengi ya kujifunza mathalani, siku moja nilimuuliza kwanini Maalim unapenda kula na mkusanyiko wa watu nyumbani? Alinijibu gharama ya kupata mawazo ya watu ni kubwa sana kuliko ya kukipata chakula.
HISTORIA
Maalim amepata elimu katika Shule ya Msingi Uondwe iliyoko Pemba na kisha akasoma Shule ya Wavulana ya Wete. Alisoma kati ya mwaka 1950 hadi1957.
Baadaye akajiunga na elimu ya Sekondari, mwaka 1958 hadi 1961 katika Shule ya Sekondari ya Kumbukumbu ya Mfalme George, iliyoko Unguja, na pia akaendelea na kidato cha tano na sita katika sekondari hiyo hiyo kati ya mwaka 1962 hadi 1963.
Maalim Seif aliyezaliwa Oktoba 22, 1943 huko Nyali Mtambwe katika Wilaya ya Wete iliyoko kisiwani Pemba, pamoja na kufaulu vema masomo ya kidato cha sita hakwenda chuo kikuu.
Ni kwa sababu serikali ilimtaka afanye kazi serikalini ili kuziba nafasi za kazi zilizokuwa wazi kutokana na kuondoka kwa wingi kwa Waingereza kurudi nchini kwao. Kwa kuanza Maalim aliajiriwa kuwa mwalimu kwa miaka tisa, kuanzia 1964 hadi 1972 akifundisha Sekondari Fidel Castro iliyoko Pemba na Chuo cha Ualimu cha Lumumba kilichoko Unguja. I
llipofika mwaka 1972 baada ya kutumikia taifa, alijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na kusomea shahada ya kwanza ya Sayansi ya Siasa, Usimamizi wa Umma na Uhusiano wa Kimataifa. Akahitimu shahada yake mwaka 1975 akawa mmoja wa wanafunzi bora waliofaulu kwa kiwango cha juu kiasi kwamba chuo kilipenda abakie kuwa mhadhiri ili afundishe, jambo ambalo hakukubaliana nalo.
ALAMA YA JUMBE
Pengine kama si uamuzi wa Rais wa awamu ya pili Zanzibar Mzee Aboud Jumbe Mwinyi, jina la Maalim Seif lingekuwapo lakini huenda lingekawia sana kufahamika, kuvuma na kusambaa kama ilivyotokea katika uhai wake. Mzee Jumbe ana alama katika maisha yake, ndiye aliyemteua kumsaidia akawa Katibu Maalum. Kisha baada ya kuona karama yake, akamteua kuwa Waziri wa Elimu.
Safari ya Maalim Seif katika mbuga ya siasa na uongozi, ikashika kasi ya ajabu na nyota yake kuanza kung’ara. Baada ya hapo akateuliwa kuwa mjumbe wa sekreteriati ya Halmashauri Kuu (NEC) CCM, akiongoza Idara ya Uchumi na Mipango hadi kufikia kuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM kwa miaka kadhaa.
Ni kazi ngumu mno kuyataja mafanikio ya kisiasa ya Maalim bila kuutaja uongozi wa mzee Jumbe na awamu yake ya pili katika serikali ya Mapinduzi Zanzibar. Jumbe ndiye kiongozi aliyeamua kuvunja mfupa kwa meno na kupitisha uamuzi wa kuwaingiza vijana wasomi katika uongozi wa serikali yake. Hapo ndipo Maalim Seif na baadhi ya wenzake walipochomoza na kuonyesha vipaji vyao wakifanyakazi pamoja na viongozi wazee na wakombozi wa Zanzibar kutoka ukoloni na kujitawala.
KUANZA HARAKATI
Maalim Seif amewahi kuwekwa kizuizini kwa madai kuwa amekutwa na nyaraka za siri za SMZ. Hata hivyo, akashinda kesi hiyo. Akiwa gerezani wenzake kadhaa wanasiasa machachari na vigogo wa Zanzibar, wakaanzisha kamati ya kupigania mabadiliko huru ya demokrasia iliyojulikana kwa jina la Kamahuru.
Walioasisi Kamahuru ni aliyekuwa Mwenyekiti Shaaban Khamis Mloo, Katibu akawa Ali Haji Pandu na wajumbe wengine akiwamo Musa Haji Kombo, Masoud Omar, Maalim Ali wa Chwaka. Wengine ni Suleiman Seif Hamad Machano, Khamisi Ali, Juma Ngwali, Dk. Maulid Makame na mwanamama pekee Jailan. Kama alivyowahi kufukuzwa CCM aliyekuwa Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar, Idara ya Fedha na Uchumi, Mansoor Yusuf Himid na NEC ya CCM, Maalim Seif pia aliwahi kukumbwa na dhoruba hiyo.
Mansoor ambaye baba yake mzazi ni kati ya wanapinduzi 14 wa ASP, sasa ni mjumbe wa Kamati Kuu ya ACT Wazalendo na mwanasiasa mstari wa mbele katika chama hicho akitokea CCM. Maalim Seif amefukuzwa ndani ya Chama Cha Mapinduzi kwa madai kuwa alikuwa na mpango ‘haramu’ wa kusuka na kuanzisha uasi wa kisiasa ndani ya chama hicho.
Hata hivyo, madai hayo hayajawahi kuwekwa bayana na kiongozi yeyote wa CCM hadi leo kama hiyo ndiyo sababu ya kufukuzwa kwake na wenzake sita. Wenzake ni pamoja na Shaaban Khamis Mloo, Ali Haji Pandu, Hamad Rashid Mohamed, Soud Yusuf Mgeni, Khatib Hassan Khatib na Suleiman Seif Hamad. Alipoachiwa huru akachaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa CUF huku naibu wake akiwa James Mapalala.
Chini ya uongozi wake, siasa za Zanzibar zilibadilika na kupamba moto kutoka mwaka 1992 kuelekea mwaka 1995, akiongoza mapinduzi ya kisiasa na harakati za vyama vingi na ushindani kwa lengo la kujenga demokrasia shirikishi. Maalim Seif pia aliwania tena urais mwaka 2000 hata 2010 pia.
Baada ya uchaguzi 2010 akawa Makamu wa Kwanza wa Rais chini ya Rais Dk. Ali Mohamed Shein na mwaka 2020 akawa Makamu wa Kwanza wa Rais Dk. Mwinyi.
Apumzike kwa amani.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED