MWANASIASA mkongwe Nicodemus Banduka (80), amepumzishwa katika nyumba yake ya milele kijijini kwake Mruma, Mwanga mkoani Kilimanjaro, wiki iliyopita.
Banduka ni kiongozi ambaye maendeleo ya wilaya ya Mwanga hayawezi kukamilika bila kutajwa jina lake, kwa kuwa ni miongoni mwa watu waliochagiza na kushuhudia kuanzishwa kwa wilaya mpya ya Mwanga mwaka ya 1979.
Banduka anapoaga dunia anatajwa na wanakijiji wengi wa Mruma kuwa ni miongoni mwa viongozi walioshika nafasi mbalimbali ndani ya chama kuanzia TANU hadi CCM na pia serikalini.
Kazi za kuhamasisha maendeleo zilifanywa kwa nguvu yake, pia wanamtaja kuwa mmoja wa vinara wa maendeleo ya kijiji chake cha Mruma na wilaya nzima.
Katika mazungumzo yake na gazeti hili jijini Dar es Salaam mmoja wa watoto wake, Davis Banduka, anasema baba yake atakumbukwa kuwa mmoja wa viongozi waliochangia kupatikana kwa wilaya ya Mwanga.
Anakumbusha kuwa kabla ya hapo Mwanga ilikuwa sehemu ya Wilaya ya Pare kisha mwaka 1979 ikazaliwa na kuwezesha Pare kuwa na wilaya mbili za Same na Mwanga ambayo ni matokeo ya juhudi za Banduka na viongozi wengine akiwamo Waziri Mkuu mstaafu, Cleopa Msuya.
Kwa mujibu wa taarifa za kiserikali, Wilaya ya Mwanga ilianzishwa Julai 1979, ikawa miongoni mwa nyingine sita zinazounda mkoa wa Kilimanjaro. Kadhalika ni jimbo la uchaguzi.
"Mzee wetu alikuwa na moyo wa kupenda maendeleo na kusaidia watu na aliwezesha kijiji chake kupiga hatua mbalimbali za kimaendeleo kwa miradi mingi tangu miaka ya 70," anasema Davis.
Davis anafafanua kuwa Kijiji cha Mruma ni cha kwanza kuwa ofisi kubwa ya chama na serikali, kuwa na mradi wa ng'ombe na pia kuwa na gari la kijiji aina ya Pick-up lililokuwa likitoa huduma mbalimbali. "Gari lilikuwa linawasafirisha wakazi wa Mruma, kuhudumia ng'ombe kwa kusombea majani, lilitumiwa pia kubeba mahindi na mazao mengine wakati wa msimu wa vuli na masika.
Lakini pia ni kijiji cha kwanza kuwa na simu za mezani na zahanati kwa juhudi za mzee Banduka," anasema Davis.
Anaongeza kuwa kijiji hicho kilikuwa cha kwanza wilayani Mwanga kuwa na maji ya bomba, umeme kuwa na shule karibu, vitega uchumi kama fremu za maduka na ukumbi wa mikutano.
"Mzee alihamasisha maendeleo ya Mruma kwa kushirikiana na watu mbalimbali akiwamo mtu mmoja anaitwa Derua. Baba ameacha alama kijijini kwake na wilayani Mwanga kwa ujumla," anasema.
Anasema mzee wake alikuwa na ushawishi mkubwa kwa wakazi wa kijiji hicho, na kwamba ilikuwa ni rahisi kuitisha kazi za ushiriki za kijamii zinazohusisha wananchi wote kwa kujitolea zinazojulikana kama 'msaragambo' kwa Kipare.
Anasema ni mhamasishaji aliyeweza kuvuta watu wakajitokeza kwa wingi kushiriki shughuli za maendeleo vijijini kwao. "Kupitia kwake mambo mengi ya maendeleo yamefanyika ingawa barabara ya kupanda milimani kijijini kwao ilichukua muda mrefu kujengwa, lakini kwa sasa imewekea lami.
Anasema miaka ya hivi karibuni alimuomba mbunge wa sasa wa Mwanga Joseph Tadayo, asaidie wananchi wenye matatizo ya kisheria jimboni ili waweze kushughulikiwa na kupata haki zao.
"Mzee alikuwa ameahidi kumpa ushirikiano, lakini kabla ya hilo halijatimia, ameondoka. Naamini mbunge ataendelea kulipa uzito na kuwasaidia wale wote wenye changamoto za kisheria," anasema.
Banduka alifahamika katika vijiji vingi na alipata sifa kutokana na kuhimiza maendeleo. Alikuwa chachu ya maendeleo katika vijiji vya Kisangara Juu, Chanjale, Vuchama Ndambwe na kote huko mbinu ya msaragambo aliokuwa akiuhimiza ilitumika kujenga barabara za vijiji ambavyo vingi vipo milimani.
NDANI YA UONGOZI
Banduka alikuwa ni kada ambaye ni miongoni mwa wajumbe wa tume ya watu 20 ambao walipewa jukumu la kuunganisha Chama cha African National Union (TANU) na Afro Shiraz Party (ASP) na kuzaliwa Chama Cha Mapinduzi (CCM), mwaka 1977.
Lakini pia anatajwa kuwa alikuwa mmoja kati ya makada 10 kutoka TANU na wengine 10 kutoka ASP walioandaa katiba ya chama kipya cha CCM, na kwamba wengi wameshatangulia mbele ya haki akibakia Pius Msekwa. Mwanasiasa huyo katika enzi ya uhai wake, amewahi kuwa mkuu wa mikoa mbalimbali ikiwamo Ruvuma, Kagera, Shinyanga na Pwani, lakini pia na mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM na anatajwa kuwa na mchango mkubwa katika siasa na maendeleo ya chama kwa ujumla.
Kada huyo anatajwa kuwa miongoni mwa wanachama waliokuwa wakizielewa vyema sera za chama hicho na kuzitangaza kwa wananchi ili waendelee kukiamini na kukipa kura kila uchaguzi unapofanyika.
Kadhalika mwaka 2005 alijitokeza kuwania ubunge wa Mwanga kupambana Profesa Jumanne Maghembe na kuleta upinzani mkali, lakini bahati mbaya kura zake hazikutosha.
Upinzani huo ulioleta ulitokana na jinsi alivyokuwa anakubalika ndani na nje ya chama kutokana na kile kinachoelezwa kuwa alikuwa mwanachama tangu angali kijana na kumfanya ajulikane zaidi.
Hata hivyo, baada ya hapo hakujitokeza tena kuwania ya ubunge na kubaki akiweka msukumo, ili CCM iendelee kushika hatamu kupitia sanduku la kura katika uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED