Mama mwenye Ukimwi, aliyeacha ARV kwa ushawishi wa maombezi

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 11:37 AM Nov 14 2024



Mwanamama Doreen Odemba.
Picha: Mtandao
Mwanamama Doreen Odemba.

“NILIACHA Dawa za Kufubaza Virusi vya Ukimwi (VVU) maarufu ARV kutokana na ushawishi wa ndugu yangu mmoja aliyenipeleka kwenye maombi,” Doreen Odemba, anayesimulia mkasa uliomkuta alipoenda kwenye maombi akiaminishwa angepona maambukizi ya virusi vya Ukimwi.

Anasema, alipofika kwenye maombi akaambiwa aache dawa, naye akatii, akifafanua aliacha kutumia dawa kwa muda na alipokwenda kupima afya, bado akakutwa kuwa na maambukizi hayo.

Doreen mwenye umri wa miaka 30 sasa, anasema baada ya hapo akapatwa na changamoto ya kiafya, alikumbwa na kiharusi kilichomsababisha kushindwa kujihudumia kwa takribani miaka miwili.

“Nilipata kiharusi, nikakonda sana nikawa wa kubebwa, hata ikafikia kujisaidia kwenye nepi kama mtoto,’’anaeleza na kuongeza kuwa: 

“Hii imenifundisha sana, sirudii kuacha dawa, niwasisitize wengine wenye hali kama yangu wasiache dawa kwa kuambiwa kwamba wameponywa.”

ALIVYOFAHAMU KAATHIRIKA

Doreen anaeleza simulizi yake kwa huzuni:“Nakumbuka dada aliyekuwa akifanya kazi za ndani nyumbani kwa mama mkubwa, alinitamkia kwa kunikaripia kutokana na utundu wangu wa kitoto. Hivi Doreen unajua kuwa wewe una Ukimwi?’

“Baada ya hapo, nilikwenda kumuuliza mama mkubwa ambaye alinijibu kuwa ni ukweli, ndiyo maana unakunywa dawa na kwamba nilizaliwa na maambukizi hayo.’

Doreen anasema alipofahamu hayo akiwa na umri wa miaka 12 na kisha kuanza kutumia dawa za kufubaza VVU mwaka 2004.

Japo haikuwa rahisi kwake kupokea kwa wepesi, Doreen anasema shuleni tayari ugonjwa huo ulikuwa ukifundishwa haikuwa vigumu kuelewa kuhusu kuwa na virusi vya Ukimwi, japo anadai ilimhuzunisha.

Doreen anasema lengo lake kubwa sasa, ni kuisaidia jamii kiujumla kutokomeza unyanyapaa, kadhalika kuwapa matumaini wenye hali kama yake kwamba, kupata maambukizi si kufa.

“Baadhi ya watu kwenye jamii si waelewa kabisa, lakini ukiwa kwenye hali hii bado unaweza kuwa na ndoto vilevile kufurahia maisha,’’anasema Doreen.

Anasema hata baada ya kuelezwa kuwa ana hali ile, baadhi ya watu walimtakia “amechoka kudanga ndo maana amejitangaza, wengine walisema ameumizwa na mapenzi si bure’.

Anasema baadhi ya ndugu walimnyanyapaa mwanzoni lakini sasa wengi wanamchukulia kawaida.

“Nakumbuka nilinyimwa fursa ya kupika chakula, baadhi ya watu waliokuwa wakifahamu kuhusu hali yangu walianza kusema pale kuwa nina virusi. Baada ya hapo nilinyimwa kazi ya upishi katika mgahawa mmoja jijini Dar es Salaam,” anafafanua.

Hata hivyo, unyanyapaa haujamkatisha tamaa. Anasema hajachoka kulizungumzia kwenye mitandao ya kijamii ambako anafurahi kukutana na watu wengi wenye hali kama yake ambao kupitia yeye wameongeza kujiamini na kujithamini.

ANATAMANI KUOLEWA

Mama huyo anasema, suala la uhusiano kwake amelipa umuhimu sana, kwa kuwa anatamani kuolewa na mtu ambaye hana maambukizi.

Pia, anarejea uzoefu wake kimaisha, anasema wanaume wasio na maambukizi wanajali afya wanapokuwa katika uhusiano na wanawake wenye maambukizi.

“Unajua mimi nina maambukizi, halafu kusema ninataka kuolewa na mwanaume mwenye maambukizi kama mimi, naona hiyo ni kujinyanyapaa.

“Hivyo nitapenda yule asiyekuwa na maambukizi ili kupunguza kujinyanyapaa,” anafafanua Doreen.

Mwanamke huyo kwa sasa akijishughulisha na ujasiriamali kumudu maisha yake, anasema unyanyapaa umezima ndoto za watu wengi wanaoishi na Virusi Vya Ukimwi.

“Ninatamani kuona jamii ikishirikiana na serikali na taasisi nyingine za kiraia kutoa elimu sahihi ya VVU,” anashauri.

Kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Kimataifa la Kupambana na Ukimwi (UNAIDS), asilimia 44 ya maambukizi mapya ya VVU yanawaangukia wanawake na wasichana na kila wiki kuna wanawake, vijana na wasichana 4,000 duniani kote huambukizwa VVU na kati yao, 3,100 wapo nchi za Afrika zilizo Kusini mwa jangwa la Sahara, kunakopatikana Tanzania na Kenya, aliko Doreen.

·          Kwa mujibu wa BBC