MARIA Maladukwa (42) mkazi wa Kijiji cha Ghidika mkoani Manyara, ametoroka kijijini humo na kukimbilia mkoani Singida kwa madai ya kufanyiwa ukatili wa kijinsia na mume wake.
Inadaiwa kuwa mume wake huyo alimfunga seng'enge na nondo ndogo katika miguu yake kama mtumwa kwa miezi miwili.
Mwanamke huyo ambaye amedhoofika mwili kutokana na mateso aliyodai kupewa na mume wake, alifika katika kijiji cha Matumbo, wilaya ya Singida huku akiwa na seng'enge katika mguu wa kushoto baada ya kutembea kwa saa 13 kutoka mkoani Manyara.
Mwenyekiti wa kijiji cha Matumbo, Juma Maloda, akizungumza na gazeti hili jana, alisema walimpokea Maladukwa juzi katika ofisi za kijiji hicho saa 11:00 jioni.
Alisema baada ya kumpokea, walimpa chakula na kwenda kulala nyumbani kwa Mwenyekiti wa Kitongoji cha CCM, Abeid Ntandu.
Maloda alisema katika maelezo yake, mwanamke huyo alidai kuwa alifanikiwa kutoroka nyumbani kwake baada ya kukata seng'enge alizokuwa amefungwa katika mguu wa kulia na kubakia na za mguu wa kushoto.
Alisema mwanamke huyo ametembea kwa miguu kwa zaidi ya saa 13 akiwa na seng'enge na nondo ndogo vilivyobaki kwenye mguu wa kushoto kutoka mkoani Manyara hadi Singida kwa ajili ya kuwatafuta wazazi wake, ambao alidai wako eneo la Makurungu.
Mwanamke huyo alidai kuwa wakati akipatiwa mateso hayo, mume wake amekuwa akimwambia alimuoa ili aje apate utajiri wa magari na mifugo na kumlazimisha kushiriki kwenye vitendo vya uhalifu, vikiwamo wizi wa mahindi kwenye mashamba ya watu.
Kutokana na mateso hayo, ameomba msaada wa serikali kwa kuwa usalama wake uko hatarini iwapo mwanamume huyo ambaye amefahamika (majina tunayahifadhi kwa sasa) atapata taarifa za kuwapo kijijini hapo.
Mwenyekiti wa kijiji hicho alisema amekwisha wasiliana na polisi kuhusu tukio hilo na taratibu za kumsaidia zinafanywa na serikali.
Machi, mwaka huu, katika kikao cha kujadili vitendo vya ukatili wa kijijisia, Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Queen Sendiga, alisema matukio ya ukatili mkoani humo yamefikia 8,360 hadi Desemba, 2023.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED