MTOTO Grayson Kanyenye (6), anadaiwa kuuawa kwa kupigwa na kitu kizito kichwani wakati mama yake akiwa matembezini usiku wa kuamkia Sikukuu ya Krismasi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, George Katabazi, akizungumzia tukio hilo, alisema mwili wa mtoto huyo ulikutwa ndani ya nyumba ukiwa na majeraha shingoni.
Katabazi alisema tukio lilitokea majira ya saa 1:00 asubuhi katika Mtaa wa Bwawani, Ilazo Extension jijini Dodoma, nyumbani kwa Ofisa Uvuvi wa Mtera, Hamis Mohamed.
Alisema, Mohamed na mama wa mtoto huyo, walitoka kwenda matembezini na kumwacha chini ya usimamizi wa dereva bodaboda wa maeneo ya Ilazo Extension jijini hapa, aliyejulikana kwa jina la Kelvin Gilbert.
Kamanda Katabazi alisema bodaboda huyo walimfahamu kupitia huduma ya usafiri anayoitoa kwa familia hiyo.
“Bodaboda huyu aliachiwa mtoto ili amwangalie kipindi ambacho watakuwa kwenye matembezi wawili hao wakati wa usiku lakini waliporudi, mtoto hawakumuona hadi asubuhi majira ya saa 1:00 walipomkuta kwenye chumba akiwa ameuawa huku akiwa na alama za kupigwa na kitu kizito shingoni mwake,” alisema.
Kamanda Katabazi alisema Jeshi la Polisi mkoani hapa linamshikilia bodaboda huyo kwa uchunguzi zaidi wa tukio hilo.
“Tumemkamata bodaboda huyo kwa ajili ya uchunguzi wa tukio hili. Yeye amekanusha kuhusika na jambo hili lakini tunaendelea na uchunguzi ili kubaini nini hasa kilitokea kwa mtoto huyu na kusababisha kifo chake,” alisema Katabazi.
Aidha, Kamanda Katabazi alitoa wito kwa wazazi kuacha kuwaachia tabia ya kukabidhi watoto wao kwa watu ambao hawawajui vizuri ili kuepusha matukio kama hayo.
“Wazazi wanapaswa kuwa makini na watu wanaowaachia watoto wao kwa ajili ya kuwaangalia hawa walimwamini bodaboda na kumwachia mtoto wakati wao wanakwenda kutembea usiku lakini kilichotokea mtoto amepoteza maisha,” alisema.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED