WATU 12 wamefariki dunia kwa ajali za magari na wengine kujeruhiwa wakati wa Sikukuu ya Krismasi katika mikoa ya Tanga na Lindi.
Mkoani Tanga, ajali ya gari iliyotokea juzi saa 3:00 usiku, watu 11 walifariki dunia na wengine 13 kujeruhiwa baada ya lori aina ya Mitsubishi Fuso lililokuwa likitokea Lushoto kwenda Dar es Salaam, kugongana na basi dogo aina ya Toyota Coaster lililokuwa likitokea Mkata kwenda jijini Tanga.
Ajali hiyo ilitokea ikiwa ni siku moja baada ya Desemba 25, mwaka huu, majira ya saa 12:00 asubuhi katika barabara ya Chalinze – Segera na watu wanane kufariki dunia papo hapo na wengine 8 kujeruhiwa baada ya magari mawili kugongana uso kwa uso. Ajali hiyo ilihusisha lori la mizigo lenye Usajili T 707 EBZ na basi dogo aina ya Toyota Coaster lenye Usajili T 497 DZW.
Juhudi za kumtafuta Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Kamishna Msaidizi (ACP) Almachius Muchunguzi, ziligonga mwamba kutokana na simu zake kutokupatikana.
Hata hivyo, Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Wakili Albert Msando, alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo apokaririwa na vyombo ya habari jijini Tanga.
"Watu 11 wamefariki dunia, wakiwamo madereva wa magari yote mawili na majeruhi 13 wamepelekwa katika Hospitali ya Wilaya ya Handeni kwa ajili ya kupata huduma ya matibabu. Kati yao, majeruhi tisa hali zao si nzuri na madaktari wanaendelea na juhudi za matibabu", alisema Msando katika taarifa hiyo.
MWINGINE LINDI
Mtu mmoja amefariki dunia na wengine saba wakazi wa Kigamboni, Dar es Salaam wamepalekwa katika Hospitali ya Mkoa wa Lindi Sokoine kwa matibabu, baada ya gari walilokuwa wakisafiria kwenda kijiji na kata ya Ng’apa mkoani Lindi kupata ajali na kupinduka.
Kwa mujibu wa maelezo kutoka kwa baadhi ya majeruhi hao na kuthibitishwa na uongozi wa Hosptali na Jeshi la Polisi, ajali hiyo ilitokea juzi eneo la Machole Manispaa ya Lindi saa 3:00 usiku.
Wakizungumzia ajali ilivyotokea, baadhi ya majeruhi hao, Tabu Mchapo, Rahma Abdallah na Rukia Issa, walisema walikuwa wanatoka Dar es Saalam kwenda kijijini kwao Ng’apa kwa ajili ya kusheherekea Krismasi na Mwaka Mpya.
Majeruhi hao walisema wakiwa wanasafiri na gari lao binafsi aina ya Toyota Noah (bila kutaja namba zake) likiendeshwa na kaka yao, Selemani Panuli, walipofika eneo la Machole mbele yao waliona mwanga mkali na kumpoteza mwelekeo kaka yao na kupinduka.
“Mimi nilikaa mbele na kuona mwanga mkali lakini si wa magari wala pikipiki na kuzimika kisha gari ikajipiga na kupinduka zaidi ya mara tatu na kusimama,” alisema Tabu.
Alisema baada ya gari kutulia, dereva alikuwa ametoka kwenye kiti chake na kichwa chake kulala juu ya miguu yake bila kumtambua kwamba alikuwa tayari ameshafariki dunia.
Tabu aliyeumia kichwani alisema wakiwa wanahangaika kujaribu kujiokoa, lilipita gari la halmashauri na kuwapa msaada wa kufikishwa Hosptali ya rufani ya Mkoa ya Sokoine kupatiwa matibabu.
“Ndani ya gari tulikuwa watu wanane na watoto wetu wanne tukienda kwetu Ng’apa kula sikukuu ya Mwaka Mpya,” alisema Tabu.
Rahma, aliyevunjika mkono wa kushoto, alisema alikuwa amekaa nyuma na kumpakata mtoto. Alisema baada ya mwanga huo kupotea, giza nene lilijitokeza na kusababisha dereva apoteze mwelekeo na kupinduka huku wengine wakichomoka na kutupwa nje.
Hassan Lukanda, Muuguzi Wodi Na. 4 walikolazwa majeruhi hao, alisema walipokea majeruhi hao saa 5:0 usiku na kwamba hali zao zilikuwa zinaendelea kuimarika kutokana na tiba wanazozipata katika hospitali hiyo.
Somoe Mnumba, mhudumu chumba cha kuhifadhia maiti, alisema akiwa nyumbani saa 5:30 usiku, alipigiwa simu kwa ajili ya kuchukua mwili wa Panuli kwa ajili ya kuuhifadhi.
Akizungumza kwa niaba ya Mganga Mfawidhi wa Hosptali hiyo, Dk. Alexander Makalla, Ofisa Habari na Uhusiano wa wa Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Lindi ya Sokoine, Pendo Mustapher, alisema walipokea majeruhi saba bila kutaja majina wakiwamo watoto wanne kati yao watatu wanawake na mwanamume mmoja.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Lindi, Kamishna Msaidizi (ACP) John Imori, alikiri kutokea kwa ajali hiyo huku akiwataka madereva kuwa makini wanapokuwa wanaendesha vyombo vya moto ili kuepuka ajali.
“Ni kweli taarifa ya ajali hiyo ninayo lakini nashindwa kuelezea kwa urefu kwani niko nje ya ofisi,” alisema Imori.
· Imaendikwa na Boniface Gideon (Handeni) na Saidi Hamdani (LINDI)
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED