TIMU ya Soka ya Taifa ya vijana wa umri chini ya miaka 17 (Serengeti Boys), wanakutana na Uganda katika mechi ya fainali ya Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati (CECAFA U-17), itakayochezwa leo kwenye Uwanja wa Hamza Nakivubo jijini Kampala, Uganda.
Serengeti Boys na Uganda zimefuzu kushiriki Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON U-17), zitakazopigwa Machi, mwakani nchini Morocco.
Serengeti Boys ilifuzu fainali hizo baada ya kuitwanga Sudan Kusini mabao 4-0, shukrani kwa Hussein Mbegu, Abel Joasiah na Ng'habi Zamu huku Uganda Cubs, ikiwachapa Somalia magoli 4-1 katika michezo yao ya hatua ya nusu fainali.
Kocha Mkuu wa Serengeti Boys, Agrey Morris, amesema wachezaji wake wako kamili kwa ajili ya mchezo huo aliotabiri utakuwa mgumu.
"Tupo kamili, wachezaji wapo katika hali nzuri na morali ya hali ya juu kwa ajili ya mchezo huu, kila mmoja yupo tayari kufanya kile atakachoagizwa akipatiwa nafasi. Tunacheza mechi ya fainali, ni muhimu, tunaomba sapoti ya Watanzania ili tuchukue kombe hili.
Ni wazi haitakuwa mechi rahisi kwa sababu Uganda wana timu nzuri sana na watakuwa nyumbani, pamoja na hilo hatuwahofii, tutapambana," alisema nahodha huyo wa zamani wa Tanzania (Taifa Stars).
Naye mchezaji timu hiyo, Saleh Ally, aliwaahidi Watanzania wajiandae kuwapokea wakiwa wanarejea nyumbani na kombe.
"Tunawaahidi Watanzania mechi hii tutafanya kila linalowezekana ili turudi Tanzania na ubingwa, nasema hivyo kwa sababu wachezaji tumejipanga kuhakikisha tunashinda mechi hii," alisema mchezaji huyo.
Awali timu hizo zilikuwa pamoja katika Kundi A na mechi yao ya hatua hiyo ilimalizika kwa sare ya bila kufungana, lakini kila mmoja akipata ushindi dhidi ya yosso wa Kenya.
Kundi B katika mashindano hayo lilikuwa na Sudan Kusini, Somalia na Sudan.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED