WAJUMBE wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii, wamepatiwa mafunzo ya namna Mfumo wa utoaji huduma kupitia mtandao PSSSF Kidijitali unavyofanya kazi.
Mafunzo hayo ambayo pia yalihudhuriwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Ridhiwani Kikwete, yamefanyika Februari 12, 2025 kwenye majengo ya bunge jijini Dodoma.
Wataalamu wa PSSSF, wakiongozwa na Mkurugenzi Mkuu, Abdul-Razaq Badru, walieleza hatua kwa hatua namna ya kujiunga na Mfumo huo kupitia Simu janja, Kishikwambi au computa.
Katika neno lake la utangulizi, Kikwete amebainisha kuwa mfumo wa utoaji huduma kupitia mtandao (PSSSF Kidijitali) ulizinduliwa wakati wa maadhimisho ya huduma ya PSSSF akitambulisha ugeni wa PSSSF kwa Kamati hiyo amesema mfumo wa utoaji huduma kwa njia ya mtandao ulizinduliwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati wa sherehe za PSSSF kutimiza miaka mitano na unamuwezesha mwachama kujihudumia mwenyewe wakati wowote mahala popote.
Akieleza jinsi mfumo huo unavyofanya kazi, Mkurugenzi wa Uendeshaji PSSSF, Mbaruku Magawa, amesema mfumo huo ni mkombozi wa waajiri, wanachama na wastaafu kwani kwa kutumia simu janja, kishikwambi au komputa, wanaweza kujiandikisha, kufatilia michango yao, kuwasilisha madai mbalimbali na wastaafu kupitia simu janja wanaweza kujihakiki.
“Kupitia PSSSF Kidijitali, wanachama wetu wanaweza kupata taarifa mbalimbali zikiwemo, michango yao, uwekezaji, kuanzisha madai mbalimbali na kuyafuatilia hatua kwa hatua, wastaafu nao wanaweza kujihakiki kupitia simu janja, lakini pia waajiri kupitia tovuti ya Mfuko wanaweza kusajili wanachama wapya, kuwasilisha michango na kupata risiti.” amefafanua Magawa.
Aidha, Mfumo wa PSSSF unaungana na mifumo mingine ya serikali kuhakikisha taarifa zinasomana.
Kwa upande wao wajumbe wa kamati hiyo wameipongeza PSSSF kwa kupiga hatua hiyo na kushauri kuboresha zaidi huduma hiyo ianze kupatikana katika simu za kawaida ambazo sio simu janja kuwezesha watu wengi zaidi kuitumia na pia kuendelea kutoa elimu kwa watumiaji namna ya kutumia huduma hiyo.
Kabla ya kuendeshwa mfunzo hayo, Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF Abdul-Razaq Badru na ujumbe wake walipata fursa ya kusalimiana na Katibu wa Bunge, Baraka Leonard.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED