WAZIRI wa Habari Utamaduni, Sanaa na Michezo Prof. Palamagamba Kabudi, amekemea tabia ya baadhi ya watangazaji kuharibu lugha ya kiswahili wakati wa utangazaji na kuirusha kwenye hadhira.
Amebainisha hayo leo, Februari 13, 2025 wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Vyombo vya Utangazaji nchini, ulioenda sambamba na maadhimisho ya siku ya Redio Duniani, Mkutano ambao umeandaliwa na TCRA, kwa siku mbili.
Amesema sekta ya utangazaji ni muhimu sana katika kuhabarisha umma taarifa mbalimbali na hata serikali imekuwa ikitumia vyombo vya habari kufikisha ujumbe wake kwa wananchi, lakini kumekuwa na matumizi ya maneno ya lugha ya kiswahili ambayo siyo fasaha.
"Vyombo vya habari muhimu sana na ni kiungo kati ya wananchi na serikali, hivyo mnapotangaza tumieni maneno kwa ufasaha ya lugha ya kiswahili na sanifu na siyo "kubananga" na kutamka Apa..badala ya Hapa, Huyu na siyo uyu," amesema Prof.Kabudi.
"Acheni kufubaza kiswahili, kukidumaza kwa kuyapa maneno ya kawaida ya Kiswahili, maana isiyo stahili.na matokeo yake nchi nyingine zimeanza kusema Watanzania ni watumiaji wa lugha ya kiswahili, lakini kiswahili chao siyo fasaha," ameongeza.
Amevikumbusha pia vyombo vya habari hasa redio viwe vinaandaa vipindi vyenye tija vya kuelimisha jamii, ikiwamo na namna ya kukabiliana na madiliko ya tabianchi na kwamba hivi karibuni maudhui mengi yamejikita kwenye mziki, michezo na burudani.
Katika hatua nyingine, amezungumzia kauli mbiu ya Mkutano huo ambayo inasema ‘Wajibu wa vyombo vya utangazaji kuelekea uchaguzi Mkuu wa 2025’, amewasihi waandishi wa habari, watumie taaluma zao kusimamia haki na usawa katika kuhabarisha umma na kuzingatia weledi sheria na kanuni za utangazaji.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Maudhui, Saida Muki, amewasisitiza waandishi wa habari kuwa makini na matumizi ya Akili Mnemba AI katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu, ili wasitoe maudhui yenye kupotosha umma.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Dk. Jabir Bakari, amesema wameandaa mkutano huo, ili kujadili masuala ya sekta ya habari, pamoja na kutafuta ufumbuzi wa changamoto ambazo bado zinaikabili sekta hiyo.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED