Miradi ya miundombinu ya elimu na afya katika Manispaa ya Geita, ambayo ilianza kujengwa kati ya mwaka 2018 na 2021 lakini haikukamilika kutokana na changamoto za kifedha, sasa inatarajiwa kukamilika ndani ya miezi mitatu ijayo. Hii ni baada ya Kampuni ya Uchimbaji Madini ya Geita (GGML) kuridhia kutoa shilingi milioni 422 kwa ajili ya kuikamilisha.
Miundombinu hiyo ni sehemu ya miradi inayotekelezwa kwa fedha za uwajibikaji kwa jamii (CSR) zinazotolewa na GGML.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Geita, Yefred Myenzi, akizungumza kwenye baraza la madiwani, amesema kuna miradi 34 ambayo inajumuisha vyumba vya madarasa, zahanati na nyumba za watumishi, ambayo haikukamilika kutokana na bajeti kuwa ndogo.
"Tulikaa na GGML na kuwaomba waridhie kutupatia Shilingi milioni 422 ili tuikamilishe. Bahati nzuri, wamekubali na sasa miradi hiyo itakamilika ndani ya miezi mitatu," amesema Myenzi.
Ameeleza kuwa kukamilika kwa miradi hiyo kutaondoa malalamiko ya wananchi, huku GGML ikiwa kwenye mchakato wa kupata wakandarasi kwa ajili ya miradi ya CSR ya mwaka 2024, ambapo miradi yenye thamani ya shilingi bilioni 5.2 itatekelezwa.
Kuhusu hali ya elimu katika Manispaa hiyo, Myenzi amesema changamoto kubwa ni upungufu wa vyumba vya madarasa na madawati kutokana na ongezeko kubwa la wanafunzi. Halmashauri inatumia mapato ya ndani kutatua tatizo hilo.
Kwa mfano, shule za msingi zenye jumla ya wanafunzi 78,000 zinahitaji vyumba vya madarasa 998. Kutokana na ufinyu wa bajeti, ujenzi unafanyika kwa awamu.
"Kila mwaka tunajenga vyumba vya madarasa na kutengeneza madawati, lakini kutokana na ongezeko la watoto, changamoto hii haiwezi kuisha mara moja. Tunahitaji kuanzisha shule mpya ili kupunguza msongamano," amesema Myenzi.
Ofisa Elimu Sekondari, Rashid Muhaya, amesema ongezeko la wanafunzi limeongeza upungufu wa madarasa, viti, meza, matundu ya vyoo, pamoja na walimu.
Hata hivyo, amesema tayari walimu wapya 42 wa masomo ya sayansi wamepangiwa kufundisha kwenye shule zenye mahitaji makubwa.
Akitolea mfano, amesema Shule ya Sekondari Nyanza ina wanafunzi zaidi ya 2,000 lakini ina madarasa 36 pekee, wakati kiwango kinachotakiwa kwa idadi hiyo ni madarasa 42. Kwa sasa, Manispaa inatafuta eneo jipya kwa ajili ya kujenga shule nyingine ili kupunguza msongamano wa wanafunzi.
Baraza hilo limempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuipandisha hadhi Halmashauri ya Geita kuwa Manispaa, ombi ambalo lilikuwa likisubiriwa kwa muda mrefu.
Akifunga kikao hicho, Mwenyekiti wa Baraza, Constantine Morandi, amewataka watumishi kuhakikisha wanatekeleza miradi ya CSR, miradi inayotokana na mapato ya ndani, pamoja na ile inayofadhiliwa na serikali kuu kwa uadilifu ili kuleta maendeleo kwa wananchi.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED