DC Mtambule apongeza ongezeko la pensheni PSSSF

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 06:56 PM Feb 13 2025
 DC Mtambule apongeza ongezeko la pensheni PSSSF.
Picha:Mpigapicha Wetu
DC Mtambule apongeza ongezeko la pensheni PSSSF.

Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, jijini Dar es Salaam, Saad Mtambule, amepongeza ongezeko la asilimia 2 ya pensheni ya kila mwezi kwa wastaafu wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF).

Pongezi hizo amezitoa baada ya kuelezwa utekelezaji wa Kikokotoo kilichoboreshwa alipotembelea Banda la PSSSF kwenye Maonesho ya Miaka 20 ya Bodi ya Mikopo kwa Wanafunzi wa Elimu ya Juu yanayoendelea katika viwanja vya Biafra wilayani humo, Februari 13, 2025.

Pia, ameipongeza PSSSF kwa kutoa huduma zake kidijitali, ambapo mwanachama wa Mfuko huo, anaweza kujihudumia yeye mwenyewe kupitia simu janja, kishikwambi au computer wakati wowote mahali popote.

"Nawapongeza sana kwa maboresho mliyofanya, hili ni jambo jema sana; Lakini pia niwapongeze kwa mfumo huu wa huduma mtandao, kupitia mfumo huu mwanachama anapata huduma instantly." amepongeza.

Akimueleza Mkuu huyo wa Wilaya kuhusu huduma mtandao (PSSSF Kidijitali), Afisa Uhusiano wa PSSSF, Coleta Mnyamani amesema, huduma hiyo imepokelewa vizuri na wanachama, kwani imeondoa ulazima wa mtu kusafiri kufuata huduma katika ofisi za PSSSF badala yake kupitia PSSSF Kidijitali mwanachama anaweza kupata taarifa za michango yake, taarifa za mafao, taarifa za uwekezaji, kuwasilisha madai mbalimbali na kwa wastaafu kupitia simu janja wanaweza kujihakiki.

Kuhusu Kikokotoo kilichoboreshwa, Mkuu huyo wa Wilaya aneelezwa kuwa, kuanzia Januari 2025, pensheni ya wastaafu imepanda kwa asilimia 2.

Aidha, Mfuko utatoa "ubani"  (funeral grant) wa shilingi laki 500,000/=, endapo Mstaafu anayepokea pensheni PSSSF atafariki.

Pia, Mstaafu akifariki, wategemezi wake wanaotambuliwa chini ya sheria ya Mfuko, watalipwa Mkupuo wa miezi 36 ya pensheni ya mwezi ya mwanachama husika.