Serikali imetoa zaidi ya shilingi bilioni 5 kuboresha miundombinu na kununua vifaa tiba vya kisasa katika Hospitali ya Taifa ya Akili Mirembe ili kuboresha huduma kwa wananchi.
Akizungumza jijini Dodoma kuhusu mafanikio ya miaka minne ya Rais Samia Suluhu Hassan, Mkurugenzi Mtendaji wa hospitali hiyo, Dk. Paul Lawala, amesema fedha hizo zimetumika kujenga majengo ya wagonjwa wa dharura na mahututi, vyumba 20 vya madaktari, nyumba za watumishi, ukarabati wa majengo 21, na ujenzi wa uzio wa hospitali.
Aidha, hospitali inaendelea na ujenzi wa maabara ya kisasa na Kituo cha Matibabu ya Uraibu kwa kushirikiana na Mamlaka ya Kuzuia na Kudhibiti Dawa za Kulevya (DCEA) chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Pia, inatarajia kukamilisha Kituo cha Ubora cha Masuala ya Afya ya Akili (National Center of Excellence for Mental Health).
Dk. Lawala ameongeza kuwa idadi ya madaktari bingwa wa afya ya akili imeongezeka kutoka watatu mwaka 2020 hadi 15, huku wengine saba wakikaribia kumaliza masomo yao chini ya ufadhili wa Samia Scholarship kupitia Wizara ya Afya.
Kwa sasa, hospitali inahudumia wastani wa wagonjwa 50,000 kwa mwaka, ambapo asilimia 60 ni wa huduma za afya ya akili na asilimia 40 ni wenye magonjwa ya mwili.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED