Askofu awajia juu viongozi wanaojikweza

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 10:05 AM Dec 27 2024
Askofu wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Mara, George Okoth.
Picha:Mtandao
Askofu wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Mara, George Okoth.

ASKOFU wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Mara, George Okoth, amewataka viongozi wa serikali, siasa, dini na kimila kuacha kujikweza na kujiinua bali wawe wanyenyekevu na kuihudumia jamii ipasavyo.

Askofu Okoth alisema hayo jana katika ibada ya shukrani ya Sikukuu ya Kuzaliwa kwa Kristo (Krismasi), maarufu kama ‘Boxing Day' iliyofanyika mjini Musoma hapa. 

Alisema viongozi wa ngazi zozote wanatakiwa kuiga mfano wa Yesu Kristo ambaye alikuja na dhana ya tofauti katika utawala, akijifanya mtu anayewatumikia watu na wala si watu kumtumikia yeye.

 "Yeye anataka kiongozi ajione kama mtumishi anayetumika kwa ajili ya watu wengine, si kutumika kwa ajili ya maslahi yake ambapo watu watahamisha mawazo yao kuwaona kwamba viongozi ni watu wakubwa, mabosi pia wako tofauti na wao," alisema Askofu Okoth.

Alisema jamii wanayoitumikia ndiyo iliwapa kibali cha kuwa viongozi kutokana na  asilimia kubwa wanapigiwa kura na wananchi, hivyo kuwataka  kuwa na utii kwa kuwasikiliza na kuwahudumia bila kujikweza.

AKEMEA UKATILI 

Mchungaji Kiongozi wa Kanisa la Tanzania Missionary Revival (TMRC), Jacob Lutubija, aliwataka waamini wa kanisa hilo kuacha vitendo vya ukatili dhidi ya watoto na wanawake aliwataka kushiriki kikamilifu kudhibiti vitendo hivyo. 

Alisema kuishi kwa kumtegemea Mungu husaidia kuondoa vitendo vya ukeketaji na ndoa za utotoni kwa jamii.

 "Ukeketaji umeshamiri katika baadhi ya maeneo ya Mkoa wetu wa Mara, wazazi kuchukua mahari kwa mtoto ambae hajafika umri wa kuolewa na kukatishia masomo,uvutaji bhangi na madawa ya kulevya mambo haya maovu hata kwenye jamii hayapendezi"alisema.
 
 Alisema mbali ya kunywa na kula vyakula vizuri katika sherehe hiyo, aliwataka waumini kumruhusu Yesu azaliwe katika mioyo yao aweze kileta amani huku akitoa wito kwa jamii kutoendelea kukumbatia imani potofu na kuishi maisha yenye hofu ya Mungu.

 Mwinjilisti wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Victoria (DVN), Sylvester Mhamaka, aliwataka wazazi kutambua jukumu lao la malezi kwa watoto ili kukabiliana na mmomonyoko wa maadili. 

Alisema Mungu alimleta Yesu duniani ili kurudisha uhai wa mwanadamu kwa kuwa kiongozi katika maisha yake.

 Alisema maadili katika jamii yamebadilika wazazi wameshindwa kuwa karibu na vijana na mabinti zao ambao wanajifunza mambo maovu kwenye mitandao kupitia simu janja hali inayochangia kuwepo kwa vitendo vya usagaji na ushoga.