Rais Samia atoa milioni 10 kwa bodaboda Arusha

By Allan Isack , Nipashe
Published at 05:44 PM Dec 27 2024
Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), Mohamed Ali Kawaida.
Picha:Mpigapicha Wetu
Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), Mohamed Ali Kawaida.

Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ametoa Shilingi milioni 10 kwa Chama cha Waendesha Bodaboda Wilaya ya Arusha ili kusaidia kukamilisha utaratibu wa kuanzisha Chama cha Ushirika cha waendesha bodaboda hao.

Aidha, Rais ametoa pikipiki mbili zitakazotumiwa na viongozi wa chama hicho kwa ngazi ya wilaya na mkoa ili kusimamia na kutatua changamoto za wanachama.

Fedha hizo zilikabidhiwa leo Jijini Arusha na Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), Mohamed Ali Kawaida, wakati wa Mkutano Mkuu wa Umoja wa Waendesha Bodaboda Wilaya ya Arusha. Mkutano huo pia ulihusisha uzinduzi wa mfumo wa kidijitali wa utambuzi wa wanachama.

Kawaida, amebainisha kuwa waendesha bodaboda walikosa fedha za kukamilisha usajili wa ushirika huo, na msaada wa Rais utawasaidia kuimarisha shughuli zao. Pia amewataka waendesha bodaboda kujisimamia kwa nidhamu, kuacha matumizi ya dawa za kulevya, na kutoshiriki kwenye uhalifu.

Kiongozi huyo wa UVCCM ameagiza Jeshi la Polisi na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kuchunguza upotevu wa Shilingi milioni 200 zilizodaiwa kuchukuliwa na viongozi wa awamu iliyopita wa bodaboda. Aidha, amewataka waendesha bodaboda kutoa ushirikiano kwa vyombo vya dola ili kuzuia watu wanaotumia mwamvuli wa bodaboda kufanya uhalifu.

1

Waendesha bodaboda wametumia fursa hiyo kuiomba serikali kupunguza gharama za leseni ya udereva kutoka Shilingi 99,000 hadi 30,000 ili kuwasaidia wengi kumiliki leseni rasmi.

Pia Mbunge wa Arusha Mjini, Mrisho Gambo, amechangia Shilingi milioni 10 kwa mfuko wa chama cha bodaboda na kutoa ahadi ya zawadi ya Shilingi milioni moja kwa atakayetoa taarifa za wahusika wa upotevu wa fedha za bodaboda. Pia amemtaka Kawaida kuwasilisha malalamiko hayo kwa Rais ili wahusika wachukuliwe hatua za kisheria.

Mwenyekiti wa Bodaboda Wilaya ya Arusha, Shwaibu Hamisi, amesema wilaya hiyo ina bodaboda 12,500, huku mkoa mzima ukiwa na jumla ya bodaboda 26,000. Mwenyekiti wa Bodaboda na Bajaji Taifa, Said Chenja, ameshukuru juhudi za Rais Samia, zikiwemo kupunguza faini za bodaboda kutoka Shilingi 30,000 hadi 10,000.

Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Arusha, Dk. Wilfred Solilel, amewasihi waendesha bodaboda kuzingatia usalama barabarani na kuacha tabia za kufanya vurugu na kutoa kelele zisizofaa wakiwa barabarani.