WATEJA zaidi ya 700 kati ya 2000 wa msimu wa sita wa promosheni ya kuhamasisha malipo na manunuzi kwa njia ya kadi inayoendeshwa na Benki ya NMB ‘NMB MastaBata – La Kibabe,’ wameshajizolea kitita cha jumla cha zaidi ya Sh. Mil. 76.4, kati ya zaidi ya Mil. 300 zinazoshindaniwa kupitia droo za kila wiki.
NMB MastaBata – La Kibabe ni kampeni inayochagiza matumizi yasiyo ya pesa taslimu, ambako wateja wa NMB wanaotumia Kadi za MastaCard kuchanja kulipia huduma kwa njia ya QR Code, PoS na NMB Pay by Link, ambapo benki hiyo huwazawadia kila wiki, kila mwezi na ‘grand final’ itakayofanyika Februari 12, 2025.
Idadi hiyo ya washindi na kiasi hicho cha pesa walizoshinda, kimekuja baada ya kufanyika kwa droo ya saba, iliyofanyika Ijumaa Desemba 27, kwenye Ofisi za NMB Tawi la Tegeta, ambako Meneja wa Tawi, Magreth Lwiva, alichezesha akisimamiwa na Pendo Mfuru kutoka Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania (GBT).
Akizungumza kabla ya droo hiyo, Magreth alisema jumla ya washindi 2000 watajishindia zawadi mbalimbali zilizotengwa na benki hiyo zikiwa na thamani ya Sh. Mil. 300 na kwamba kila wiki wateja 100 hujinyakulia kiasi cha Sh. 100,000, huku wengine 40 wakishinda zawadi za papo hapo, zikiwemo vocha za manunuzi ‘shopping challenge.’
“NMB MastaBata pia hutoa zawadi za kila mwisho wa mwezi kwa miezi miwili, ambako washindi 15 hujinyakulia Sh. 500,00 kila mmoja, washindi watano hujishindia safari ya kutembelea Mguga za Wanyama za Mikumi na Ngorongoro na wengine watano kujishindia pesa hadi Sh. mil. 4 za ada zao au watoto wao.
“Katika droo ya mwisho yaani grand finale, wateja wetu sita watajishindia tiketi za kusafiri Kwenda Dubai wao na weza wao, ambapo wataka huko kwa siku tano kwenye Hoteli ya Nyota Tano, safari ambayo itagharamiwa kila kitu na NMB,” alibainisha Magreth mbele ya Afisa wa Idara ya Biashara ya Kadi NMB, Salehe Nkuruvi.
Kwa upande wake, Pendo Mfuru kutoka GBT, alisema Bodi yake inaishukuru NMB kwa namna inavyoendesha droo zake kwa uwazi na haki, huku akiwataka wateja wa benki hiyo kuwa huru wanaposhiriki droo mbalimbali, kwani inazingatia sheria, kanuni na miongozi wanayopewa na GBT.
“Niko hapa kwa niaba ya GBT, uwepo wangu hapa unalenga kuhakikisha droo inachezeshwa kwa kuzingatia vigezo na masharti yanayosimamia michezo hii, ili kupata wateja kihalali, ambalo ndilo jukumu mama la taasisi yetu. Hivyo tunawahakikishia wateja wa NMB kwamba, haki, vigezo na masharti vinazingatiwa,” alisema.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED