SIKU chache baada ya kuchaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Stephen Wasira anazungumza na Nipashe na kutangaza kile anachokilenga kuwa ni jukumu la kutangaza utekelezaji wa ilani ya uchaguzi mkuu wa chama chake ya mwaka 2020.
Anataja sababu ya kufanya hivyo kuwa ni kutaka wananchi wajue maendeleo yaliyoletwa na serikali ya CCM, katika kipindi cha miaka mitano ili chama kichaguliwe tena uchaguzi mkuu wa mwaka huu.
"CCM imetekeleza ilani yake kwa kujenga zahanati, vituo vya afya, hospitali, shule, miradi ya maji na mingine mingi ya maendeleo, hivyo ni vyema niende kwa wananchi kuwaelezea hayo," anasema Wasira.
Mwanasiasa huyo mkongwe anasema suala la kushika dola linahitaji kuwatekelezea wananchi kile ambacho umeahidi ili wakuchugue tena, na kwamba CCM imetekeleza ilani yake.
Wasira anasema ni wajibu wa CCM kuwaonyesha wananchi kile ambacho waliahidi kuwafanyia, kwa kuwa kushika dola kunatokana na ridhaa yao hasa pale ahadi za kuwaletea maendeleo zinapotimizwa.
"Lakini kwa manufaa ya Watanzania wanaotaka kunifahamu vizuri, ni vyema niwaelezee jinsi ambavyo nimekuwa ndani ya chama na serikali na utendaji kazi wangu uliotukuka," anasema.
Anasema mwaka 1970, kwa mara ya kwanza alichaguliwa kuwa mbunge akiwa na umri wa miaka 25 katika Jimbo la Mwibara, Wilaya ya Bunda, wakati huo akitokea Wilaya ya Geita alikokuwa akifanya kazi kama Katibu Mtendaji wa TANU Wilaya.
Wakati huo Sengerema na Nyangh'wale zilikuwa ndani ya wilaya ya Geita, lakini sasa nazo ni wilaya tena Geita ni mkoa.
"Kabla ya kuwa Katibu Mtendaji wa TANU wa wilaya, nilianza kazi katika Idara ya Maendeleo ya Jamii wilayani Ukerewe mkoani Mwanza kwenye Kijiji cha Mriti," anakumbusha.
MBUNGE ‘MCHANGA’
Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, anasema mwaka 1970 akiwa na miaka 25, alichagulikuwa kuwa mbunge wa Jimbo la Mwibara wilayani Bunda mkoani Mara, akiwa na umri mdogo, kisha ilipofika 1975 akateuliwa kuwa Naibu Waziri wa Kilimo.
"Mwaka huo wa 1975 niliteuliwa kuwa mkuu wa mkoa wa Mara nikiwa na umri wa miaka 30. Ilipofika 1982 hadi 1985 nilikwenda kufanya kazi katika ubalozi wa Tanzania huko Washington DC, nikapata fursa ya kusoma vyuo vikuu nikigharamiwa na Mwalimu Julius Nyerere 1985 nilichaguliwa kuwa mbunge wa Bunda," anasema.
Mkongwe huyo anafafanua kuwa mwaka 1987 Rais wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi alimteua kuwa Naibu Waziri wa Serikali za Mitaa na Vyama vya Ushirika, Mwaka 1989 hadi 1990 alikuwa Waziri Kamili wa Kilimo na Mifugo.
"Mwaka 1990 hadi 1991 niliteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Pwani, wakati nikifanya kazi hiyo ya ukuu wa mkoa huko Mara na Pwani, vilevile nilikuwa katibu wa chama cha TANU au CCM," anasema.
Anaongeza kuwa ni mzoefu ndani ya chama na serikali, na kwamba mwaka 2005 hadi 2015 ilikuwa ndani ya serikali ya awamu ya nne, na kwamba kila Baraza la Mawaziri lilipobadilishwa, bado aliniteuliwa.
"Kuwa katika serikali za awamu karibu zote, kumenipa uzoefu mkubwa wa masuala ya kitaifa na kimataifa, kufanya shughuli za serikali na chama kumeniwezesha kuijua vyema nchi yetu. Mimi ni miongoni mwa Watanzania wachache wanaoijua Tanzania ya jana ya leo na wanaozungumza Tanzania ya kesho," anasema.
WASIRA NI WA NANE
CCM imempata Makamu Mwenyekiti Taifa wa nane tangu chama hicho kilipoanzishwa mwaka 1977 baada ya kuunganishwa na Chama cha Afro Shirazi Party (ASP) cha Zanzibar.
Wasira anachaguliwa na wajumbe wa Mkutano Mkuu Maalum wa CCM Taifa jijini Dodoma wiki iliyopita ili kuziba nafasi hiyo ilioachwa na mtangulizi wake Abdulrahman Kinana.
Kabla ya Wasira, wapo makada wa CCM waliowahi kushika nafasi hiyo wa kwanza ni Aboud Jumbe Mwinyi, aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa CCM kuanzia mwaka 1977 hadi 1984.
Baadaye nafasi hiyo ilishikiliwa na Ali Hassan Mwinyi, kuanzia mwaka 1984 hadi 1990 kisha akafuata Rashid Kawawa aliyeongoza kuanzia 1990 hadi 1992. Viongozi wote hao ni marehemu.
John Malecela alifuatia akashika nafasi hiyo kuanzia 1992 hadi 2007 akamwachia Pius Msekwa mwaka 2007 hadi 2012 kisha ikawa ni zamu ya Philip Mangula 2012 hadi 2022.
Mangula aliandika barua ya kujiuzulu nafasi hiyo akielezea kuwa ana sababu binafsi ndipo nafasi yake ikachukuliwa na Kinana ambaye mwaka jana aliandika barua ya kujiuzulu nafasi hiyo.
Baada ya Kinana kijiuzulu, wajumbe wamemchagua Wasira kuwa Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara ambaye amaweka wazi jukumu alilonalo wakati huu wa kuelekea kwenye uchaguzi mkuu.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED