Wenye magonjwa makubwa wapelekwe hospitali za serikali -Rais Samia

By Beatrice Shayo , Nipashe
Published at 11:06 AM Jun 25 2024
Rais Samia akizungumza kwa njia ya simu na Mkuu wa Mkoa wa Arusha Paul Makonda.
Picha: Maktaba
Rais Samia akizungumza kwa njia ya simu na Mkuu wa Mkoa wa Arusha Paul Makonda.

RAIS Samia Suluhu Hassan amepiga simu wakati kambi maalumu ya madaktari bingwa ikiendelea jijini hapa na kuagiza watakaobainika kuwa na matatizo makubwa wapelekwe hospitali za serikali kwa matibabu zaidi.

Kambi hiyo ya siku saba iliyoanza jana iliyoandaliwa na Mkuu wa mkoa huo, Paul Makonda, walijitokeza zaidi ya watu 5,000 wakiwamo wa mikoa ya Dodoma, Kilimanjaro na Manyara.

Kutokana na idadi kubwa ya wagonjwa wamelazimika kuweka utaratibu maalum wa kuhudumia baadhi, huku wengine wakitakiwa kurudi leo na wenye shida ya tezi dume na saratani wakibaki kupatiwa utaratibu wa matibabu.

Wakati huduma hizo zikiendelea, Rais Samia alimpigia simu Makonda mubashara akitaka kujua kinachoendelea.

“Nimekupigia ulinipa taarifa kuwa leo (jana) kutakuwa na kambi ya matibabu ndani ya mkoa huu, nilitaka kujua kama hiyo kambi imefanyika,” aliuliza Rais Samia na kujibiwa imeanza na imepata madaktari na wauguzi zaidi ya 450 na dawa za kutosha huku, hospitali zote kubwa binafsi na za serikali zikiitikia wito.

“Lakini Mheshimiwa Rais Samia furaha tuliyokuwa nayo  ni kuwapo kwa helikopta ya kumbeba mwananchi wa kawaida maskini na kumpeleka hospitali yoyote nchini Tanzania kwa ajili ya kupatiwa matibabu,” alisema Makonda.

Hata hivyo, Rais Samia alipohoji kuhusu helikopta hiyo, Makonda alimweleza kwamba, wameipata kupitia wadau ambao wanahusika na utoaji wa huduma za afya mkoani humo.

“Wadau wa utalii wameunga mkono jambo hili ili kuhakikisha wananchi wanafikia huduma za afya kwa wakati baada ya kuelewa maelekezo yako na upendo uliokuwa nao kwa wananchi, hasa wanyonge na maskini ambao wanapambana na afya zao,” alisema Makonda.

Rais Samia aliwashukuru madaktari waliojitolea pamoja na waliojitolea kuleta helikopta hiyo.

“Bila shaka hapo kutatakiwa mafuta kwa waliojitolea, maombi yangu kwa wananchi wajitokeze kufanya shughuli kama hiyo, ni jambo kubwa na lina gharama, hivyo wananchi wasipojitokeza gharama zitakuwa zimeenda bure.

“Niwaombe sana wananchi wa Mkoa wa Arusha, wajitokeze watumie fursa hiyo, na mimi nipo nyuma yao, Mkuu wa Mkoa kama kuna kitu chochote ambacho kinatakiwa kama kusaidia chakula ama mafuta, basi utuambie ili tuongeze nguvu kambi iende vizuri,” alisema Rais Samia.

Pia, alisema ataangalia jambo la kufanya katika kambi hiyo kwa siku saba wanazowahudumia wananchi kuwekeza ili wananchi wapate matibabu.

Awali, Makonda alisema anatambua wapo wananchi ambao wanapata mateso katika afya na wengine kupoteza maisha, kwa sababu ya gharama kubwa za matibabu.

“Kuna wengine hawajui hata waende wapi, ili tuwe watumishi wazuri, lazima tuwatumikie hawa wananchi ukitoka hapa utapatiwa dawa, utapatiwa upasuaji bila kulipia tumekuja mbele yenu kuwatumikia ili mtukumbuke na sisi wakati wa uhitaji wetu watu wasimame kutupigania,” alisema.

 Makonda alisema kuna kipindi madereva wa bodaboda walimfuata na kumuomba mchango kwa ajili ya mwenzao aliyepata ajali na yupo hospitali anahitaji fedha ya kujitibu.

Alisema wanapokuwa na bima ya afya maana yake hawatahangaika kuchangisha watu katika kipindi ambacho wanahitaji matibabu.

Aliwaeleza kwamba, mgonjwa akayezidiwa katika kambi hiyo bila kujali ana fedha au la atapelekwa bure kwa helikopta hospitali za Mount Meru, KCMC au Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), Dar es Salaam na wenye matatizo ya macho kuna miwani ya bure 5,000.

Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Dk. Peter Kisenge, alisema wamejiandaa kutoa vipimo na matibabu ya moyo na wale ambao watahitaji usaidizi wa karibu watawasafirisha bure kwenda Dar es Salaam kwa matibabu zaidi.

WANANCHI

Josephine Masawe, alisema licha ya kuwahi, ameshindwa kupata huduma kutokana na idadi ya watu kuwa kubwa, na kutatakiwa kurejea siku inayofuata.

Elisante Yacob, alipongeza kuwapo kwa kambi hiyo ya bure ambayo inawasaidia wasiojiweza kumudu gharama hospitalini.

Alisema alipatiwa namba 337 na tayari amemwona daktari na kupewa dawa kwa ajili ya tatizo lake kutokana na kupata ajali na mkono kuvunjika na kumsababishia maumivu makali.