'Wafoji' namba kuwahi foleni kliniki ya Makonda

By Beatrice Shayo , Nipashe
Published at 12:20 PM Jun 26 2024
Zoezi la kliniki ya Makonda  likiendelea.
Picha: Maktaba
Zoezi la kliniki ya Makonda likiendelea.

BAADHI ya wananchi waliojitokeza katika kliniki ya matibabu katika Jiji la Arusha, wamedaiwa kutumia ujanja wa kutengeneza namba feki ili wapatiwe matibabu kwa haraka.

Tukio hilo limesababisha usumbufu kwa wagonjwa waliochukua namba tangu juzi na kujikuta namba zao zigongana na waliofoji na wao kuanza kuhudumiwa mapema. 

Akizungumza na wananchi waliojitokeza kwa ajili ya kupatiwa matibabu katika kliniki hiyo ya siku saba, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda, amesema wapo ambao walipatiwa namba juzi na hawajapatiwa huduma.

“Kuna watu wamejitengenezea namba zao juzi wamekuja nazo leo (jana) badala ya wale waliobaki juzi kuendelea jana, wakajikuta wamechukuliwa ambao ni wapya, sasa tumekubaliana turejee kwenye namba zilizotolewa juzi,” amesema Makonda huku wakimshangilia.

“Lengo ni kuhakikisha wale wote wa juzi ambao wamepatiwa namba wamalizike katika matibabu halafu tuendelee na watu wa leo (jana) tumeelewana?”

Aidha, amesema mpaka sasa madaktari na wauguzi wamefanya kazi kubwa idadi ya watu waliotibiwa imeenda mara tatu ya malengo waliyokuwa nayo.

“Madaktari wamefanya kazi kubwa, wametoka majira ya saa nne usiku na saa 11 alfajiri, wapo katika hivi viwanja. Ninaomba niwahakikishie wananchi wote wa Mkoa wa Arusha hakuna atakayekanyaga katika hivi viwanja asipatiwe matibabu.

“Usijisikie vibaya ukadhani kuna mtu amechukua nafasi yako haya mambo ya kuwahi na kuchukua namba ya mtu mwingine unaweza kupata ugonjwa ambao si wako ila si tabia njema kutengeneza namba bandia kutaka kuwahi jambo ambalo muda wako haujafika.

“Tuna hadi miwani tunayotoa bure, gharama yake ni Sh. milioni moja, nimefurahi kuona yule bibi alivyopatiwa miwani alikuwa anafurahia, naombeni mjitokeze pia kuna saratani ya tezi dume, nenda ukapime bure, hii fursa usiiache,” amesema.

Makonda amesema kuna baadhi wakienda kupima hospitali wanajikuta tatizo lao limefika kwenye hatua mbaya wakati angewahi kupima afya angegundulika mapema.

Aidha, amesema tayari kuna wadau wamejitolea dawa za Sh. milioni 25, Bohari ya Dawa (MSD) wametoa dawa za Sh. milioni 12 na kama kuna wengine wapo tayari kuchangia dawa na vifaa wanakaribishwa.

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Dk. Charles Mkombachepa, amesema mwitikio wa wagonjwa waliojitokeza ni mkubwa na wanaendelea kuwahudumia.

Amesema wagonjwa wengi wapo katika magonjwa ya ndani, huduma ya macho, kupima kifua kikuu, huduma za saratani.

Amesema huduma za rufani wanazitoa kwa haraka na kupatiwa matibabu katika hospitali za serikali na binafsi.

Dk. Mkombacheka amesema juzi walihudumia wagonjwa 2,034. Kati yao, wanawake 1,053 na wanaume 973.

WALALAMIKIA KUKOSA DAWA

Elizabeth Bosco, aliyefanyiwa vipimo, amelalamikia kitendo cha kupewa dawa za siku tatu badala ya siku 14.

“Nimepewa dawa nusu naambiwa dawa zimeisha sasa hizo za siku nyingine nitazipata wapi wakati sina hela ya kwenda kuzinunua hizi dawa?” alihoji.

Jack Amfrey alisema mtoto wake amebainika ana tatizo kiafya na kuandikiwa dawa za aina mbili ambazo ametakiwa kwenda kuzinunua kwa kuwa dawa zimeisha.

Mahema yenye foleni kubwa ni ya Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), hema la kuhudumia watoto, saratani, magonjwa ya ndani na huduma ya macho.